Mkuu
 wa Wilaya ya Uvinza Mwalimu Hadijah Nyembo (kulia) akitoa nasaha zake 
kabla ya kumkaribisha mgeni rasmi Mkuu wa Mkoa wa Kigoma, Luteni Kanali 
Mstaafu Issa Machibya (wa pili kulia) kuzungumza na wakazi wa wilaya ya 
Uvinza kwenye sherehe za uzinduzi wa kituo cha redio jamii Uvinza FM 
mkoani Kigoma. Kutoka kushoto ni Meneja wa huduma za kijamii wa Airtel 
Tanzania, Hawa Bayumi, Mshauri na Mkufunzi kutoka Shirika la Umoja wa 
Mataifa la Elimu, Sayansi na Utamaduni (UNESCO) ambao ndio wadhamini 
wakuu wa redio Uvinza FM, Bi. Rose Haji Mwalimu na Mkurugenzi Mtendaji 
wa Uvinza FM Radio Bi. Nuru Kalufya.(Picha na Zainul Mzige wa MOblog).
Na Mwandishi wetu, Uvinza – Kigoma
Mkuu wa Mkoa wa Kigoma, Luteni 
Kanali Mstaafu Issa Machibya amesisitiza uadilifu katika vyombo vya 
habari jamii kwa kutangaza habari zisizoumiza hisia kwa wananchi wengine
 na kuepuka migogoro.
Akizindua kituo cha redio jamii cha 
Uvinza FM, Luteni Kanali Mstaafu Machibya alisema kuwa vyombo vina 
wakati mgumu hasa katika kipindi cha kuelekea uchaguzi mkuu mwaka 2015.
“Changamoto hii inaweza kuepukika 
kwa kuhakikisha habari zinazotolewa zinalenga kuendeleza utamaduni wa 
amani, upendo, utulivu na uvumilivu na kuepuka viashiria vinavyoweza 
kusambaza chuki kwa lengo la kufanikisha chaguzi salama.
Mkuu wa Mkoa huyo amesisitiza 
umuhimu wa kuutumia uhuru wa kutoa na kupata habari vizuri kwa kusema 
kwamba uhuru huo usitumike kutoa habari zinazopendelea upande mmoja na 
kukandamiza mwingine kwa kuwa hali kama hiyo husababisha machafuko.
“Kwa mujibu wa Ibara ya 18 (b) ya 
Katiba ya Jamhuri wa Muungano wa Tanzania ya mwaka 1977, kila mtu anayo 
haki ya kutafuta, kupokea na kutoa habari bila ya kujali mipaka ya nchi,
 lakini haki hiyo iende sambamba kwa kuzingatia Sheria za nchi na 
kuhakikisha habari hizo haziumizi hisia za wananchi wengine,”
Luteni Kanali Mstaafu Issa Machibya 
ameitaka redio jamii Uvinza kuonyesha uwezo wao ili waweze kujitangaza 
na kujijengea imani kwa wanajamii wao kuwa wanaweza. “Ni kwa hali hiyo 
tu mtaweza kujulikana, kutambulika na kupata udhamini na matangazo ya 
kutosha.”
Amewataka wanajamii kukitumia vyema 
kituo chao cha redio ili kiwe chachu ya kuleta na kukuza maendeleo 
katika vijiji, wilaya, mkoa na taifa kwa ujumla.
Wakati huo huo Mkuu wa Mkoa ameitaka
 redio jamii ya Uvinza kutangaza habari zenye kuonyesha madhara ya mila 
potofu na kujenga uelewa wa jamii kuhusu mila hizo hususan mauaji ya 
watu wenye ulemavu wa ngozi (albino), kufichua wagonjwa wanaohofia kuwa 
na dalili za ugonjwa wa ebola na uharibifu wa mazingira.
Amelipongeza shirika la umoja wa 
mataifa linaloshughulikia Elimu, Sayansi na Utamaduni (UNESCO) kwa kutoa
 msaada wa vifaa vya kituo hicho na kuendesha mafunzo ya kuwajengea 
uwezo wanahabari jamii, Kampuni ya simu za mkononi ya Airtel kwa 
kuruhusu matangazo ya Uvinza FM Redio yarushwe kupitia mnara wake na 
waanzilishi wa kituo hicho.
Mwalikishi
 wa Shirika la Kimataifa la Elimu, Sayansi na Utamaduni (UNESCO) ambaye 
pia ni mshauri na mkufunzi wa redio jamii, Bi. Rose Haji Mwalimu 
akizungumza kwa niaba ya Mkurugenzi Mkazi wa UNESCO Tanzania, Zulmira 
Rodrigues kwenye sherehe za uzinduzi wa kituo hicho cha redio jamii 
Uvinza FM uliofanyika wilayani Uvinza mkoani Kigoma.
“Ninayapongeza mashirika hayo ya 
Umoja wa Mataifa na Airtel kwa ufadhili wao, Ruchugi Salt Works na Asasi
 za kiraia (EHENA) kwa ushirikiano wao kwa jambo hili”
Kwa upande wake, Mkuu wa Wilaya ya 
Uvinza Mwalimu Hadijah Nyembo amewakumbusha waandishi wa habari kuepuka 
kutangaza habari zinazoleta hofu katika jamii kwa kutangaza habari 
zinazotoa maelezo ya ufafanuzi kutoka chombo husika.
Amekemea matumizi ya lugha isiyo 
sahihi na kutoeleweka kwa wasikilizaji kwa kusema kwamba redio inalenga 
makundi yote ya umri kwa hiyo Matangazo yalenge wananchi wote.
“Redio Uvinza isiwe chombo cha 
propaganda, zingatieni mojawapo ya madhumuni ya kuanzishwa kwa redio 
zenu ambayo yanalenga kuhamasisha mshikamano, Amani, upendo, utulivu, 
umoja na utaifa, alisema Mwalimu Nyembo.”
Chombo cha habari jamii Uvinza FM Redio ni cha kwanza kuanzishwa mkoani Kigoma katika halmashauri mpya ya Uvinza.
Chombo hicho kimetakiwa kutumika 
kuwaunganisha wanajamii, kuepuka kutangaza hisia au uvumi kwa kueleza 
ukweli na kuwatunzia heshima wasikilizaji wao kwa kuwa wana haki ya 
kuheshimiwa na kutoumbuliwa masuala yao binafsi.
Uzinduzi huo umeshuhudiwa pia na 
Mkuu wa wilaya ya Uvinza Mheshimiwa Mwalimu Hadijah Nyembo, viongozi wa 
chama na serikali, viongozi wa dini, Shirika la Umoja wa Mataifa 
(UNESCO), Kampuni ya simu za mkononi AIRTEL, wanakijiji na wananchi wa 
halmashauri ya Uvinza.
Wengine ni wanahabari 30 
wanaohudhuria mafunzo ya maadili, jinsia na habari za migogoro kijijini 
Uvinza, kutoka redio jamii za wilaya 8 ambazo ni Karagwe, Bunda, Mwanza,
 Kahama, Sengerema, Maswa, Simanjiro, Loliondo, Mpanda, Ngara. Kutoka 
Zanzibar ni Unguja North, na Southern Pemba (Pemba).
Meneja
 wa huduma za kijamii wa Airtel Tanzania, Hawa Bayumi, akitoa salamu kwa
 wakazi wa wilaya ya Uvinza kutoka kampuni ya simu za mkononi ya Airtel 
ambao wametoa udhamini wa mnara wao kurusha matangazo ya kituo cha redio
 jamii Uvinza FM ili kupanua wigo wa usikivu kwa redio hiyo.
Mkurugenzi
 Mtendaji wa Uvinza FM Radio Bi. Nuru Kalufya akitoa neno la shukrani 
kwa mkuu wa mkoa na wadhamini wa kituo hicho cha redio jamii Uvinza FM.
Meneja
 wa huduma za kijamii wa Airtel Tanzania, Hawa Bayumi akishiriki kutoa 
burudani na kikundi cha wakinamama wachimba chumvi Uvinza.
Mkuu
 wa Mkoa wa Kigoma, Luteni Kanali Mstaafu Issa Machibya akikata utepe 
kuashiria uzinduzi rasmi wa kituo cha redio jamii Uvinza FM chini ya 
ufadhili wa Shirika la UNESCO na kampuni ya simu za mkononi ya Airtel 
Tanzania. Wanaoshuhudia tukio hilo kutoka kulia ni Meneja wa huduma za 
kijamii wa Airtel Tanzania, Hawa Bayumi, Mwalikishi wa Shirika la 
Kimataifa la Elimu, Sayansi na Utamaduni (UNESCO) ambaye pia ni mshauri 
na mkufunzi wa redio jamii Bi Rose Haji Mwalimu pamoja na Mkurugenzi 
Mtendaji wa Uvinza FM Radio Bi. Nuru Kalufya.
Mkuu
 wa Mkoa wa Kigoma, Luteni Kanali Mstaafu Issa Machibya akifanyiwa 
mahojiano mafupi ndani ya studio za redio jamii Uvinza FM na Mtangazaji 
wa kituo hicho, Kadisilaus Simon mara baada ya kuzindua rasmi redio 
hiyo.
Mkuu wa Mkoa wa Kigoma, Luteni Kanali Mstaafu Issa Machibya akisaini kitabi cha wageni ndani ya studio za redio jamii Uvinza FM.






No comments :
Post a Comment