MCHEZA filamu maarufu wa kike nchini, Yvonne Cherry ‘Monalisa’ ameziponda tuzo za Min Ziff Red Carpet kwa madai kuwa, hazina hadhi.
Monalisa amesema tuzo hizo zilizotolewa hivi karibuni kwa wachezaji filamu nchini, zilikuwa za ubabaishaji na maandalizi yake yalikuwa ya zimamoto.
Mwanadada huyo alisema hayo wiki iliyopita kupitia mtandao wa filamucentre baada ya kuulizwa mtazamo wake kuhusu utoaji wa tuzo hizo.
“Kusema ukweli, tuzo zilizotolewa hazikuwa na hadhi ya tuzo kutokana na maandalizi yake,”alisema msanii huyo wa zamani wa kundi la Mambo Hayo.
Mbali na tuzo zilizotolewa kutokuwa na hadhi, Monalisa alisema maandalizi ya utoaji wake yalikuwa ya zimamoto kutokana na kushindwa kufanyika kwa wakati uliopangwa.
Alisema ratiba iliyotolewa na waandaaji wa tuzo hizo ilionyesha kuwa, shughuli ingeanza saa mbili usiku, lakini badala yake ilianza usiku wa manane.
“Ni kweli wasanii tunahitaji tuzo au motisha kutoka kwa wadau wetu, wanaoguswa na kazi zetu, lakini jambo hili linahitaji maandalizi na tukio zima kupewa hadhi inayotakiwa,”alisema.
“Kwangu mimi, hafla ya utoaji wa tuzo hizo niliiona kama tamasha tu, ambalo halina tofauti na matamasha mengine yanayoandaliwa kila kukicha,”aliongeza. Monalisa amezishauri mamlaka zinazohusika na utoaji wa vibali kwa waandaaji wa tuzo mbalimbali, kuwa makini kwa kutowapa vibali hivyo watu wasiokuwa na sifa na uwezo.
Alisema wapo watu makini na wenye sifa za kuandaa tuzo hizo, lakini mamlaka husika zimekuwa zikiwanyima vibali kwa kisingizio cha kuwepo kwa watu maalumu wenye haki hiyo.
No comments :
Post a Comment