Na Peter Mwenda
CHAMA cha Wananchi (CUF) kimevuna wanachama 1,108 kutoka Chama cha Mapinduzi (CCM), CHADEMA na wanachama wapya katika wilaya ya Kilwa.
Naibu Mkurugenzi wa Mipango, Uchaguzi Siasa na Bunge, Bw. Shaweji Mketo alisema katikia ziara hiyo ya wiki moja wananchi wa wilaya hiyo wametaka mabadiliko ya kutatatua kero mbalimbali zinazowakabili.
Bw. Mketo alisema CUF imebaini kuwa wananchi hao wanakabiliwa na matatizo makubwa ya kutokuwa na vituo vya afya, soko la zao la ufuta, elimu na ukosefu mkubwa wa maji.
"Kilwa ina historia kubwa Tanzania lakini inakabiliwa na matatizo mengi ya ukosefu wa maji safi na salama,hakuna zahanati katika Kata nyingi na hapakuwa na soko la zao la ufuta kabla ya Mbunge Kilwa Kusini (CUF) Bw. Selemani Bungala kutafuta soko ambako sasa kilo moja inauzwa mpaka kufikia sh. 1,700" alisema Bw.
Alisema katika ziara hiyo mbayo ilihusisha Kata za Kandawale, Njinjo, Ruhatwe, Kibata, Chumo, Kinjumbi na Kilwa Masoko kuna uhaba mkubwa wa walimu na kutoa mfano katika shule ya Sekondari ya Kibata tarafa ya Kipatimu ayenye wanafunzi zaidi ya 400 lakini kuna walimu watatu tu.
Bw. Mketo alisema CUF imejenga ngome imara katika mikoa ya Kusini na hasa wilaya ya Kilwa ambako kuna Mbunge kupitia chama hicho Bw. Suleiman Bungala "Bwege".
Alisema katika mikutano yao ilifanyika karibuni katika Kata Nane za Wilaya Kilwa wamevuna wanachama kutoka CCM (395)Chadema (38) na wengine ambao hawakuwa wanachama wa chama chochote 675.
Alisema wananchi wa wilaya hiyo wamejenga imani na CUF hivyo chama hicho kimejipanga kutatua matatizo ya wananchi katika huduma mbalimbali za maji, elimu, afya, miundombinu na ujenzi wa maabara katika shule za msingi na Sekondari.
Wakati huo huo Bw. Mketo alisema matokeo ya utafiti wa Synovate wa kuonesha kuwa kama ungefanyika uchaguzi Mkuu sasa hivi upinzani unachukua madaraka ya nchi hiyo inaonesha watanzania wanataka mabadiliko.
Alisema pamoja kuwa Synovate inaonesha kuwa CHADEMA inapewa nafasi kubwa ya kuchukua madaraka lakini ifikapo mwaka 2015 watanzania wanataka kuona mabadiliko ya uongozi na si CCM.
No comments :
Post a Comment