Amir Mhando |
KAMATI ya
Utendaji ya Chama cha Waandishi wa Habari za Michezo Tanzania (TASWA) ilikutana
Dar es Salaam Ijumaa Septemba 27, 2013 kujadili masuala mbalimbali chini ya
Mwenyekiti wa chama hicho, Juma Pinto.
(A) MKUTANO WA KATIBA/UCHAGUZI
MKUU
Kikao kilikubaliana
sekretarieti ya TASWA ishirikiane na Kamati ya Katiba ya TASWA inayoongozwa na
Mhariri Mtendaji wa gazeti la Mwanaspoti, Frank Sanga kuhakikisha mchakato wa
Rasimu ya Katiba mpya ya chama hicho unaenda vizuri.
Kamati hiyo ya katiba itasimamia mchakato huo na
ihakikishe kabla ya Desemba 15 mwaka huu, rasimu hiyo iwe tayari na ikabidhiwe
kwa Kamati ya Utendaji ya TASWA, ambayo itaiwasilisha kwenye Mkutano Mkuu wa Katiba
wa chama utakaofanyika Desemba 21 mwaka huu, mahali patakapotangazwa.
Hata hivyo Kamati
ya Utendaji imeiagiza sekretarieti ya TASWA kujipanga vizuri ili kuhakikisha mkutano
wa kujadili Katiba unafanyika nje ya Dar es Salaam kuwezesha wajumbe wawe
watulivu zaidi na kufanya uamuzi sahihi kuhusiana na katiba yao.
Pia kikao hicho
kimepanga Uchaguzi Mkuu wa TASWA ufanyike Januari 18 mwakani jijini Dar es
Salaam. Utaratibu zaidi kuhusiana na uchaguzi huo utatangazwa, lakini si dhambi
wala si nongwa kwa wanaotaka kuingia madarakani wakianza kutangaza nia mapema.
Pia wanachama wametakiwa kulipia ada zao kabla ya Novemba 30 mwaka huu.
(B) TUZO ZA WANAMICHEZO BORA
Chama chetu kila
mwaka kimekuwa kikiendesha tuzo za Wanamichezo Bora, lakini mwaka huu
tumechelewa kutokana na sababu mbalimbali, ikiwemo baadhi ya wadhamini
waliokubali awali kutusaidia kushindwa kutekeleza ahadi zao.
Hata hivyo suala
hilo sasa limepatiwa ufumbuzi na
Jumatano Oktoba 2, 2013, Mwenyekiti wa TASWA, Juma Pinto atafanya mkutano na
waandishi wa habari kwenye mgahawa wa City Sports Lounge, Dar es Salaam saa
tano asubuhi kuzungumzia suala la tuzo pamoja na kutangaza tarehe ya kufanyika
kwake. Atakuwepo pia Mwenyekiti wa Kamati ya Tuzo, Haji Manara.
(C) MAFUNZO
Kama mnavyofahamu TASWA na Shule
Kuu ya Uandishi wa Habari na Mawasiliano kwa Umma (SJMC) ya Chuo Kikuu cha Dar
es Salaam (UDSM) wameingia ushirikiano ya kuendesha mafunzo kwa waandishi wa
habari za michezo nchini.
Kuna muelekeo mzuri kuhusiana na
jambo hilo, ambapo vyombo hivyo vinaendelea na mazungumzo na wadhamini zaidi
kwa nia ya kuyafanya mafunzo hayo yawe bora na tayari wapo waliojitolea
kutusaidia ingawa ingawa si kwa bajeti yote.
(D)
Uchaguzi Mkuu wa TFF
Kikao
kilijadili kwa kina suala la uchaguzi wa TFF na kuweka jambo hilo kiporo kwanza
na kufanyia kazi baadhi ya changamoto, hadi Jumanne Oktoba 1 mwaka huu, ambapo
kikao kingine cha Kamati ya Utendaji kitafanyika.
(E)
UANACHAM WA AIPS
TASWA
ni mwanachama hai wa Chama cha Waandishi wa Habari za Michezo Duniani (AIPS)
chenye makao yake makuu Lausanne, Uswisi na kila mwaka tumekuwa tukishiriki
kwenye mikutano, lakini wanachama wetu asilimia kubwa hawana kadi za AIPS kwa
vile si wanachama.
Faida za kadi hizo unaweza kutumia viwanja vya michezo mbalimbali
duniani ambako kuna vyama vya waandishi wa habari za michezo.
Naomba
kuwajulisha kuwa utaratibu wa kupata kadi za AIPS kwa mwaka 2014 tayari
umeanza, hivyo kila mmoja kwa nafasi yake aombe kwa njia ya mtandao huu:http://www.aipsmedia.com/ index.php?page=getcard.
Ukishakubaliwa fomu yako utaelekezwa
uwasiliane na TASWA, ambapo utapewa utaratibu wa malipo ambayo ni dola za
Marekani kumi (10) tu, ambapo gharama za utumaji wa ada hizo kwa fedha za
kigeni kabla ya Novemba mosi mwaka huu chama kitaingia.
Lakini baada ya muda huo kupita, wale ambao
watachelewa kujaza fomu bado watakuwa nayo nafasi ya kupata kadi hizo, ila
watalazimika kuingia gharama za kutuma fedha za kigeni nje, ambazo chama
hakitabeba tena jukumu hilo.
Nawasilisha.
Amir Mhando
Katibu Mkuu TASWA
29/09/2013
No comments :
Post a Comment