Rais Jakaya Kikwete |
DAR ES SALAAM, Tanzania
Rais Dk. Jakaya Kikwete amemtumia Salamu za Rambirambi Waziri wa Habari, Vijana, Utamaduni na Michezo, Dk. Fenella Mukangara kufuatia kifo cha msanii maarufu wa kujitegemea hapa nchini, Juma Kilowoko maarufu kwa jina la kisanii la Sajuki, kilichotokea usiku wa kuamkia tarehe 2 Januari, 2013 katika Hospitali ya Taifa ya Muhimbili alikokuwa amelazwa kwa matibabu.
Enzi za uhai wake, Marehemu Juma Kilowoko alianza kujishughulisha na Tasnia ya Sanaa kwa kujiunga na kundi maarufu la sanaa la Kaole kabla ya kufanya uamuzi wa kuwa msanii wa kujitegemea ambapo aliendelea kupata umaarufu katika tasnia ya michezo ya kuigiza na filamu na kufanikiwa kutengeneza filamu nyingi.
Baada ya kuanza kuugua mwaka 2010, Marehemu Kilowoko aliwahi kupatiwa matibabu nchini India mwaka 2011 na kurejea akiwa amepata nafuu kubwa kiasi cha kumwezesha kutengeneza filamu nyingine, lakini alianza kuugua tena hadi mauti yalipomkuta.
Taarifa iliyotolewa na Ikulu jijini Dar es salaam, leo, imemkariri Rais Kikwete akisema kuwa amesikitishwa na kuhuzunishwa mno na kifo cha Msanii Juma Kilowoko ambaye ametoa mchango mkubwa katika kuinua kiwango cha sanaa hususan michezo ya kuigiza na filamu hapa nchini.
"Kwa hakika kifo cha msanii huyu ni pigo kubwa kwa Tasnia ya Michezo ya Kuigiza na Filamu ambayo inaendelea kujizolea umaarufu mkubwa miongoni mwa Watanzania”, amesema Rais Kikwete katika Salamu hizo za Rambirambi.
“Kutokana na msiba huu mkubwa, nakuomba wewe Waziri wa Habari, Vijana, Utamaduni na Michezo, Dk. Fenella Mukangara unifikishie salamu zangu za rambirambi na pole nyingi kwa Familia ya Marehemu Juma Kilowoko kwa kuondokewa na Kiongozi na Baba wa Familia.
“Natambua uchungu ilio nao Familia ya Marehemu Kilowoko, lakini nawahakikishia kwamba binafsi niko pamoja nao katika kuomboleza kifo cha mpendwa wao. Nawaomba wawe na moyo wa uvumilivu, ujasiri na subira katika kipindi hiki kigumu cha maombolezo. Namuomba Mwenyezi Mungu, Mwingi wa Rehema aipokee na kuilaza mahala pema peponi roho ya marehemu Juma Kilowoko, Amina”.
Aidha Rais Kikwete ametoa pole kwa wasanii wote nchini hususan wanaojishughulisha na masuala ya michezo ya kuigiza na filamu kwa kumpoteza mwenzao na hivyo kuleta simanzi na huzuni kubwa miongoni mwao. Hata hivyo amewataka kuwa wavumilivu na kuchukulia kifo hiki kama changamoto kwao katika kuendeleza tasnia ya michezo ya kuigiza na filamu hapa nchini.
No comments :
Post a Comment