MCHEZO WA MASUMBWI, TAA INAYOZIZIMA – SEHEMU YA SABA
Na Onesmo Ngowi
Masumbwi
au kwa majina mwengine ndondi au ngumi na kwa majina ya mitaani ndogwa,
mawe n.k. ni mchezo unapoendwa sana na watu wengi. Aidha mchezo huu ni
kati ya michezo inayoogopwa sana duniani. Mchezo wa ngumi uko hatarini
kupoteza maana yake ya asili yaani kucheza kama burudani, kuwakilisha
nchi na kujenga ushupavu wa mchezaji. Mamilioni ya watu wanaojazana
kuutazama wasingependa kabisa kujiingiza kuucheza mchezo wa ngumi. Sasa
endelea………………………………….!
Ni
katika miaka ya 40 hadi 70 ambapo mchezo wa ngumi ulivuma sana kwa
kutoa mabondia waliosheheni kila aina ya sifa na viwango vizuri vya
ngumi. Katika kipindi hiki mashirikisho mengi ya ngumi yalianzishwa na
sheria za ngumi pamoja na mifumo yake kubadilika.
Athari
nyingi alizokuwa anapata bondia ulingoni zilirekebishwa. Kwa mfano
sheria nyingi zililenga kumlinda bondia asidhurike na ngumi alizokuwa
anapigwa.
Glovu
zilitengenezwa za uzito tofauti na zilizowekwa pamba za kuzuia maumivu
makali kwa bondia. Nazo kofia (Head Guards) za kuzuia kichwa kisiumie
sana nazo zilianza kutengenezwa na kutumika kwenye mazoezi ambayo mara
nyingi ndiyo yanayomuumiza sana bondia kutokana na raundi nyingi
anazocheza kwenye sparing!.
Kwa
kawaida bondia anatakiwa apigane wastani wa raundi zisizopungua 100 kwa
wiki wakati anapojiandaa na mpambano. Mara nyingi anatakiwa apigane na
mabondia wenye uzito kuliko yeye ili apate usugu na uzoefu wa kuhimili
makonde ya mpinzani wake.
Wapo
mabondia wengi waliojizolea sifa kemkem katika kipindi hiki na kuwa
mashujaa wa jamii. Kwa kuwa wengi wa mabondia hawa walitoka nchi za
Amerika ya Kaskazini na Ulaya waliweza kujulikana sana kwa uwezo wa
vyombo vyao vya habari.
Ni
kweli kwamba nchi nyingine za Afrika na Asia kulikuwa pia na mabondia
wetu waliong’ara katika kipindi hiki kama vile bondia Dick Tiger wa
Nigeria ambaye alitokea kuwa tishio kwa mabondia wengine duniani. Bondia
huyu alijulikana sana kwa kuwa alihamia Ulaya (Uingereza) na hivyo
ilikuwa rahisi kwa vyombo vya habari kumjua na kumtangaza.
Ukosefu
wa vyombo vya habari vilivyo na uwezo wa kutangaza dunia nzima
uliwakosesha sana mabondia wetu kujulikana ulimwenguni. Japokuwa
walikuwa wanajulikana hapa Afrika lakini hawakutajwa kabisa na vyombo
vya habari vya nchi zilizoendelea hivyo kuwanyima nafasi kubwa ya
kujulikana na mapromota wa mchezo wa ngumi.
Bondia
Joe Louis wa Marekani ambaye aliheshimika sana kwa ushupavu wake
ulingoni na maisha yaliyopendwa na wengi nje ya ulingo aliongoza kundi
hili la mabondia wa wakati wake. Joe Louis aliyekuwa mweusi alipata sana
shida kukubalika kwa Wamarekani wote kwani kipindi chake ubaguzi wa
rangi ulikuwa umeshamiri sana nchini Marekani.
Pengine
ni tabia yake ya kutopenda makuu na ujuzi wake mkubwa ndani ya ulingo
yaliyowafanya Wamarekani wa rangi zote wampende kwa kiwango kikubwa.
Akiwa
ameweka msingi mzuri uliofuatwa na mabondia wengine kama kina Sonny
Liston, Jack Dempsey, Rocky Marciano, Muhammad Ali, Floyd Paterson, Ken
Norton, Archie Moore, Jack Quary, Joe Franzier, Joe Burgner, Alexis
Anguelo, Leon Spinks,
Wengine
ni pamoja na Michael Spinks, George Forman, John Kontey, Alan Minter,
Sugar Ray Leonard, Saad Muhammad, Marvin Hugler, Larry Holmes, Tom
Heantz, Roberto Duran, Alfred Benitez na wengine wengi.
Mabondia
wengi waliotajwa hapo juu walikuwa wa uzito wa juu kwani ni uzito
uliokuwa na soko zaidi kwa wakati huo. Mabingwa wengi wa dunia
waliolipwa vizuri walikuwa wa uzito wa juu (Heavy).
Katika
bara la Afrika mabondia waliowika sana wakati huo japokuwa hawakuwa wa
uzito wa juu ni pamoja na Dick Tiger (Nigeria), Philip Waruinge, Dick
Tiger Murunga (Kenya) Titus Simba (Tanzania) John Kotey (Ghana) n.k.
Miaka ya 80 hadi 2000 Afrika iliweza kuonyesha cheche nyingi katika
medani ya kimataifa kwa kutoa mabondia wengi waliojizolea sifa kemkem.
Mabondia
hawa japokuwa hawakuwa wa uzito wa juu lakini walivuma sana kwa kutoa
upinzani mkali kwa mabondia wengi wa nchi zilizoendelea waliongozwa na
Lottie Mwale na Francis Musankabala (Zambia), Steven Muchoki, David
Attan, Michael Irungu, Robert Wangila, Isaya Ikonyi, na Modesti Napunyi
(Kenya),
Wengine
ni Emmanuel Mlundwa, Lucas Msomba, Ahmed Tesha, John Hugo, Clemence
Chacha, Isangura, Nassor Michael, Joseph Marwa, Onesmo Ngowi, Gerald
Isaac, Ali Muhamed, Emmanuel Kimaro, Rashid Matumla (Tanzania), Ayub
Kalule, John Mugabi, John Odhiambo, Boza Edward, John Byaruhanga, Mustafa Waisaja na Cuban Businge (Uganda).
Nchi
nyingi za kiafrika kama vile DRC, Ethiopia, Afrika ya Kusini, Misri na
nyingine nyingi zilikuwa na mabondia wengi waliong’ara sana katika
ulimwengu wa masumbwi. Sifa na ushupavu wa mabondia wa wakati ule ni
tofauti kabisa na wakati huu.
Miaka
ya 70 – 2000 ngumi zilichezwa sana kwa ushindani na uwakilishi wa nchi.
Mabondia wengi walipigana kufa na kupona kuwakilisha vyema nchi zao.
Ushindi ulipopatikana ulikuwa faraja kwa taifa zima na kila mwananchi
alifurahia sana ushindi huo.
Japokuwa
hapa Afrika hususan Tanzania mapambano mengi yalikuwa hayaonyeshwi
kwenye televisheni, radio nyingi zilitangaza kwa ustadi mkubwa.
Kwa
mfano kipindi cha katikati ya miaka ta 70 upinzani mkubwa wa masumbwi
katika nchi za Afrika Mashariki ulikuwa kwenye uzito wa Fly, light
welter, Welter na middle. Wanamasumbwi waliokuwa wapinzani wakubwa kwa
wakati huo ni mabondia Emmanuel Mlundwa, Lucas Msomba, William Lyimo,
Ahmed Tesha na Onesmo Ngowi toka Tanzania kwa upande mmoja.
Toka
Kenya ni mabondia Stephen Muchoki, George Findo, Modesti napunyi, David
Attan na wengine wengi (Kenya). Katika mashindano ya nchi hizi za
Afrika Mashariki mabondia hawa na wenzao wa Uganda kama kina John
Byaruhanga, John Mugabi, Ayubu Kalule, Cuba Businge, Mustafa Waisaja na Bonza Edward waliufanya mchezo wa ngumi kuwa na upinzani mkubwa sana.
Mchango
mkubwa waliotoa mabondia hawa katika kuuendeleza mchezo wa ngumi
unafahamika japokuwa ni tuzo chache sana zilizokwisha tolewa kwao.
Lakini sio tabia ya waafrika kuwatuza watoto (wanamichezo) wake.
Inafahamika kuwa katika bara al Afrika Nanabii hawaheshimiki kwao!
Nina imani kubwa kuwa mabondia hawa wataingizwa kwenye ECAPBF “Hall of Fame” ikiwa ni juhudi za ECAPBF kuwaenzi wale waliochangia kwenye maendeleo ya ngumi katika ukanda huu. Iaendelea………………………….!
No comments :
Post a Comment