Uongozi wa Kampuni ya Reli
Tanzania –TRL unafuraha kuwataarifu wateja wake na wananchi kwa ujumla
kuwa huduma ya usafiri wa treni ya Jiji ambao ulikuwa umesitishwa kwa
wiki tatu zilizopita kuanzia Machi 24, 2013, itaanza tena hapo kesho
Aprili 22, 2013.
Kuanza tena kwa huduma hiyo
kumetokana na kukamilika kwa kazi ya ukarabati wa awali wa eneo la tuta
la reli Tabata Mwananchi lililokuwa limeathiriwa na mvua kubwa hapo
Machi 24, 2013.
Wahandisi wa Kampuni Hodhi za Mali
na Uendelezaji wa Miundombinu ya Reli-Rahco walikabidhi eneo hilo kwa
Wahandisi wa TRL hapo mchana Aprili 19, 2013. Halikadhalika ukarabati wa
kuimarisha eneo hilo utaendelea kufanywa na Rahco.
Kwa mujibu wa ratiba ya treni ya
jiji safari hizo zitaanza kama kawaida hapo kesho saa 12:30 asubuhi
kutoka kituo cha Ubungo Maziwa na kuishia Kituo cha Reli cha Dar es
Salaam ambapo huduma ya awamu ya kwanza itamalizika kama kawaida saa 5
asubuhi.
Aidha awamu ya jioni itaanza saa
10 kutokea Kituo cha Reli Dar kwenda Ubungo Maziwa kupitia vituo saba
vikiwemo Kamata, Buguruni Bakhresa, Buguruni kwa Mnyamani, Tabata
Matumbi, Tabata Mwananchi , Mabibo na kuishia Ubungo Maziwa. Huduma ya
jioni humalizika saa 4 usiku.
Hakuna mabadiliko ya nauli kila
mtumiaji wa huduma atatakiwa kulipia Shilingi 400 kwa mtu mzima na
watoto na wanafunzi Shilingi mia moja kwa safari moja.
Imetolewa na Ofisi ya Uhusiano kwa niaba ya Mkurugenzi Mtendaji wa TRL,
Mhandisi Kipallo Aman Kisamfu.
Dar es Salaam,
Aprili 21, 2013
No comments :
Post a Comment