Mechi
namba 163 ya Ligi Kuu ya Vodacom iliyochezwa juzi (Aprili 28 mwaka huu)
kwenye Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam na kumalizika kwa Simba kuibuka
ushindi wa mabao 2-1 dhidi ya Polisi Morogoro imeingiza sh. 18,014,000.
Watazamaji
3,145 walikata tiketi kushuhudia mechi hiyo ambayo viingilio vilikuwa
sh. 5,000, sh. 8,000, sh. 15,000 na sh. 20,000 huku kila klabu ikipata
mgawo wa sh. 3,564,252.45 wakati Kodi ya Ongezeko la Thamani (VAT)
iliyolipwa ni sh. 2,747,898.31.
Kiingilio
cha sh. 5,000 ndicho kilichovutia watazamaji wengi ambapo waliokata
tiketi hizo walikuwa 2,841 na kuingiza sh. 14,205,000 wakati idadi ndogo
ya washabiki ilikuwa ya kiingilio cha sh. 20,000 kilichovutia washabiki
36 na kuingiza sh. 720,000.
Mgawo
mwingine wa mapato hayo ni asilimia 15 ya uwanja sh. 1,812,331.75,
tiketi sh. 3,183,890, gharama za mechi sh. 1,087,399.05, Kamati ya Ligi
sh. 1,087,399.05, Mfuko wa Maendeleo ya Mpira wa Miguu (FDF) sh.
543,699.53 na Chama cha Mpira wa Miguu Mkoa wa Dar es Salaam (DRFA) sh.
422,877.41.
LIGI KUU YAINGIA RAUNDI YA 25
Ligi
Kuu ya Vodacom (VPL) inaendelea katika raundi yake ya 25 kesho (Mei
Mosi) kwa mechi tano zitakazochezwa katika miji ya Dar es Salaam,
Turiani, Morogoro na Mlandizi.
Licha
ya kuwa tayari Yanga imetawazwa kuwa mabingwa wa VPL msimu huu
(2012/2013), mechi dhidi ya Coastal Union itakayochezwa Uwanja wa Taifa,
Dar es Salaam ni moja kati ya zitakazovuta macho na masikio ya
washabiki wa mpira wa miguu nchini.
Mechi
hiyo namba 172 itachezeshwa na mwamuzi Simon Mberwa kutoka Pwani
akisaidiwa na Said Mnonga na Charles Chambea wote wa Mtwara wakati
mwamuzi wa mezani atakiwa Hashim Abdallah wa Dar es Salaam. Kamishna wa
mechi hiyo ni David Lugenge kutoka Iringa.
Viingilio
katik mechi hiyo itakayoanza saa 10.15 jioni ni sh. 5,000 kwa viti vya
rangi ya bluu na kijani, sh. 8,000 kwa viti vya rangi ya chungwa, sh.
15,000 kwa VIP C na B wakati VIP A itakuwa sh. 20,000. Tiketi zitauzwa
uwanjani siku ya mchezo.
Mtibwa
Sugar itakuwa mwenyeji wa African Lyon katika mechi namba 170
itakayochezeshwa na mwamuzi Dominic Nyamisana wa Dodoma kwenye Uwanja wa
Manungu ulioko Turiani mkoani Morogoro. Nayo Kagera Sugar iliyo katika
nafasi ya tatu kwenye msimamo wa ligi hiyo itakuwa mgeni wa Polisi
Morogoro kwenye Uwanja wa Jamhuri mjini Morogoro.
Uwanja
wa Azam Complex ulioko Chamazi, Dar es Salaam na wenye uwezo wa
kuchukua watazamaji 7,000 uko tayari kwa mechi kati ya JKT Ruvu na
Tanzania Prisons. Nayo Ruvu Shooting itakuwa nyumbani kwenye uwanja wake
Mabatini ulioko Mlandizi, Pwani kuikabili Oljoro JKT kutoka Arusha.
MTANZANIA APEWA ITC KUCHEZA MSUMBIJI
Shirikisho
la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF) limetoa Hati ya Uhamisho wa Kimataifa
(ITC) kwa mchezaji Yusuf Kunasa kucheza nchini Msumbiji.
Shirikisho
la Mpira wa Miguu cha Msumbiji (FMF) lilituma maombi TFF kumuombea hati
hiyo Kunasa anayekwenda kujiunga na timu ya Estrela Vermelha da Beira
inayocheza Ligi Kuu nchini humo.
Kunasa
ambaye msimu huu hakuwa na timu (free agent) amejiunga na timu hiyo
akiwa mchezaji wa ridhaa (amateur). Zaidi ya wachezaji kumi kutoka
Tanzania hivi sasa wanacheza katika klabu mbalimbali nchini Msumbiji.
No comments :
Post a Comment