NA MWANDISHI WETU
CHAMA
Cha Mapinduzi (CCM) kimeipongeza serikali, kwa uamuzi wake kurejesha
bungeni kwa ajili ya mdajala zaidi, muswada wa sheria ulioanzisha kodi
mpya ya tozo ya sh. 1,000 kwa laini ya simu.
Taarifa
ya CCM iliyotolewa leo mjini Dodoma, na Katibu wa NEC ya CCM, Itikadi
na Uenezi, Nape Nnauye imesema uamuzi huo umedhihirisha kwamba serikali
inawasikiliza na kuwajali wananchi wake.
Akiripotiwa
na baadhi ya vyombo vya habari leo, Waziri wa Fedha, Dk. William Mgimwa
amekaririwa akisema kwamba mjadala kuhusu muswada wa sheria ya kodi
hiyo ya tozo hiyo utafanyika wakati wa mkutano wa Bunge unaotarajiwa
kufanyika mwishoni mwa mwezi Agosti mwaka huu.
Baada
ya kupitishwa na bunge Juni mwaka huu, na utekelezwaji wake kuanza
rasmi Julai mwaka huu, CCM ilikuwa miongoni mwa wadau waliopinga vikali
kuanzishwa kwa kodi ya tozo hiyo, ikieleza kwamba ni mzigo na usumbufu
usio wa lazima kwa watumiaji wa simu ambao wengi matumizi yao ni ya
kawaida.
Katika
taarifa hiyo, CCM imesema kwa kuwa wabunge wengi ni wa chama hicho,
watumie fursa hiyo kuhakikisha sheria ya tozo hiyo inaondolewa na wakati
huohuo watumie uwezo wao wote kuhakikisha wanaishauri serikali vizuri
kupata njia mbadala itakayotumika kuziba nafasi itakayokuwa imeachwa kwa
kuondolewa tozo hiyo.
"Kimsingi
hatua hii imetupa faraja na hivyo CCM inaipongeza Serikali kwa kuamua
kusitisha sheria ya kodi ya tozo hiyo ya sh. 1,000 kwa laini ya simu kwa
kuwa ingesababisha usumbufu na adha isiyo ya lazima kwa wananchi",
imesema CCM katika sehemu ya taarifa yake.
No comments :
Post a Comment