Utangulizi
Katika madaraka yote ambayo Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania
imetoa kwa Bunge kwa mujibu wa ibara ya 63, wajibu wa ‘kuisimamia Serikali’
ndio wajibu unaoelezea hasa kazi za Kamati za Bunge. Ni kupitia Kamati za Bunge, za kisekta au za mahesabu, Serikali huwajibika kujieleza kinaga ubaga
kuhusu mipango yake,kuomba fedha na kuelezea matumizi ya Fedha hizo.
Mfumo wa utendaji kazi wa Kamati za Bunge ni mfumo ambao unaweza
kuimarisha uwajibikaji nchini na hivyo rasilimali za nchi kutumika vema na
kuendeleza wananchi. Mfumo dhaifu wa Kamati za Bunge huipa fursa Serikali
kufanya itakavyo na kuimarisha ufisadi kama vile matumizi matumizi mabaya ya
madaraka, wizi, udanganyifu,hongo,uzembe uvivu.
Mada hii itajikita katika maeneo ya kuzingatia ili kuwezesha Kamati za Bunge
kusimamia misingi ya Uwajibikaji na hivyo kuzuia ufisadi na kuelekeza rasilimali za
nchi kwenye maeneo ya Maendeleo ya wananchi badala ya anasa na
kutajirisha kundi dogo la viongozi.Tutaona majukumu ya Kamati katika
kusimamia Fedha za Umma na maeneo muhimu sana ya kuweka kipaumbele
katika usimamizi huo. Tutaona changamoto za Kamati na namna ya kuzitatua ili
kuwezesha Bunge kutekeleza wajibu wake inavyopasa.
UWAJIBIKAJI
Demokrasia ya kibunge ni moja ya mfumo wa kutazamana kati ya Tawi la
Utendaji (tunaita Serikali), Tawi la Uwakilishi (Bunge) na Tawi la utekelezaji wa
Sheria (mahakama). Demokrasia inajumuisha uwajibikaji katika matumizi ya
madaraka (McGee, D 2002). Uwajibikaji ni pamoja na kuweka mifumo ya
kuwezesha maamuzi kufanyika kwa namna ambayo uadilifu unazingatiwa na
kwa ufanisi. Uwajibikaji unapaswa kuhusisha matawi yote ya Serikali na jamii kwa
kupitia asasi za kiraia na vyombo vya habari.
Ibara ya 63 ya Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania imegawa
madaraka kwa Mhimili wa Bunge ambapo majukumu matatu makuu
yameainishwa, nayo ni Uwakilishi, Kuisimamia Serikali na Kutunga sheria. Kwa
kupitia mambo kama kuuliza maswali kwa mawaziri na maswali ya papo kwa
papo kwa Waziri Mkuu, kuwasilisha hoja binafsi,kuwasilisha miswada binafsi na
kujadili miswada ya Serikali, hoja ya kuahirisha Bunge nk, Bunge huweza
kuifanya Serikali kuwajibika kwayo. Kamati za Bunge mahesabu – Kamati ya
Hesabu za Serikali, Kamati ya Hesabu za Serikali za Mitaana Kamati ya Bajeti, ni
muundombinu muhimu sana katika kuhakikisha kuwa Serikali inajieleza na kujibu
hoja kuhusu sera zake na namna inavyotekeleza sera hizo, maombi ya fedha na
matumizi ya fedha hizo ili kufanikisha sera za Serikali.
Uwajibikaji hauna lengo tu la kukamata watu wanaovunja sheria bali unalengo
la kuweka mfumo ambapo kila mtu mwenye mamlaka anajibu kwa matendo
yake na hata pale asipotenda ikiwa alitakiwa kutenda ( answerable to actions
and inactions). Uwajibikaji unajenga tabia ya watu, na hasa watu wenye
mamlaka, kuzingatia Katiba, Sheria, kanuni na taratibu katika kufikia maamuzi
yao.
Iwapo mtu mwenye mamlaka akifanya jambo ambalo hawezi kulitetea mbele
ya umma, au analionea aibu kulielezea, ni dalili kubwa kwamba jambo hilo au
uamuzi huo unatokana na rushwa. Uwajibikaji unaweza mfumo ambao kila mtu mwenye mamlaka atapaswa kujielezea na kutetea uamuzi wake hadharani. Kwa mfano, Waziri anapochukua uamuzi fulani wa kisera akijua kuwa ni lazima
uamuzi ule aujibie maswali ndani ya Bunge, itamfanya Waziri huyo afanye
uamuzi mzuri na wenye maslahi kwa Taifa. Lakini kama Waziri huyo anaweza ‘kuwaona’ wabunge fulani na kuwataka wamlinde kwa uamuzi huo ni dhahiri uamuzi huo ni wa kutilia mashaka maana jambo jema halihitaji kulindwa.
Hivyo wakati mwingine uwajibikaji huonekana kufanyika ilhali ufanisi haupo kwani
sehemu fulani ya Wabunge inakuwa imeamua kutetea jambo lolote linaloletwa
na Waziri aliyezungumza kabla na wabunge. Hii ndio hatari kubwa sana
inayokabili mabunge mengi duniani.
Wakati kila mwaka Kamati ya Bajeti inapaswa kusimamia uwajibikaji katika
mapato ya Serikali (finance bill) na mgawanyo wake (appropriation bill), Kamati
za Mahesabu zina wajibu wa kutumia sheria hizo kuhakikisha (i) makusanyo ya
fedha hizo yamekusanywa kama ilivyoombwa na kuidhinishwa na Bunge na (ii)
Matumizi ya Fedha hizo yamefanyika kama ilivyoidhinishwa na kwa kuzingatia
thamani ya fedha (value for money).
KAMATI ZA BUNGE ZA MAHESABU
Kamati za Bunge za Mahesabu ni asasi muhimu za Bunge katika kuhakikisha
Serikali inawajibika kwa wawakilishi wa wananchi. Majukumu ya kamati hizi
yameainishwa na Kanuni za Bunge, nyongeza ya nane.
Kama tutakavyoona
katika kiambatanisho cha mada hii, majukumu yote yanahusisha kazi
iliyofanywa na Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG). Nyaraka
muhimu na ya kwanza katika kazi za Kamati za kusimamia mahesabu ni Ripoti
ya Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali. Hivyo Kamati za Bunge za mahesabu na CAG wanapaswa kufanya kazi kwa pamoja na kwa ushirikiano
mkubwa sana. Ndio maana Bajeti ya CAG inapitishwa na Kamati ya PAC na
ikishapitishwa hakuna mamlaka ya kuhoji tena. Vile vile PAC ndio Kamati yenye
mamlaka ya kuteua Mkaguzi wa kukagua mahesabu ya Ofisi ya CAG.
Ni wajibu wa Kamati za Bunge za mahesabu kulisaidia Bunge katika kuiwajibisha
Serikali. Mara kadhaa kumekuwa na maelezo kwamba kazi ya Bunge ni
kuishauri Serikali, hapana. Katika kuisimamia Serikali ndani yake kuna kuna
ushauri hivyo ushauri haupaswi kuwekewa mkazo zaidi ya usimamizi. Warasimu
wa Serikali wanapenda neno ushauri na kuchukia neno usimamizi. Wabunge hawapaswi kuingia katika mtego wa ‘kazi yao ni kushauri’ kwani huo ni mtego
uliotegwa na warasimu ili kupunguza nguvu ya Bunge. Kazi ya Bunge ni
kusimamia Serikali. Kamati za Bunge za mahesabu ndio zenye kubeba mzigo
huo mkubwa sana kwa niaba ya Bunge
.Hivyo tutaona ni namna gani uadilifu ni jambo la msingi sana katika wajibu huu. Vilevile ndio maana ni rahisi sana kuona Kamati za Mahesabu zikipewa kila aina ya shutuma kutoka kwa wasimamiwa
na wakati mwingine kwa kuwatumia baadhi ya Wabunge kwa kujua au
kutokujua.
Wakati mwingine Kamati za Bunge huambiwa kuangalia ‘mahesabu tu’ basi. Ni
wajibu wa Kamati za Bunge kuangalia mahesabu ya Umma na kuona kama
matumizi ya Fedha za Umma yanafanikisha malengo yaliyotarajiwa
(performance audit). Itakuwa ni uwendawazimu kwa Kamati kuridhika kwa
kuangalia tu mizania ya Serikali au Mashirika ya Umma au Serikali za Mitaa. Kwa
mfano ni wajibu wa Kamati kuangalia kama Fedha zilizotolewa kwa ujenzi wa
Barabara zimetumika kwa kazi hiyo. Ni wajibu zaidi wa kamati kuangalia kama
gharama hiyo iliyotumika kujenga barabara husika ndio gharama halisi na sio
kwamba imezidishwa ili kunufaisha watu wachache. Ni wajibu mkubwa zaidi wa
kamati kaungalia kama barabara hiyo imejengwa kwa kiwango kinachotakiwa.
Hii inaitwa ‘value for money’.
Katika utendaji wa Kazi hizi ni muhimu na lazima, Kamati za Bunge kutumia
kwanza Taarifa ya Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali. Hata hivyo
Kamati pia zaweza kutumia taarifa kutoka vyanzo vingine mbalimbali kama
wananchi na vyombo vya habari katika kufikia malengo ya kuchunguza. Kwa
mfano, hivi karibuni moja ya Magazeti hapa nchini (Gazeti la Jamhuri) liliandika
kuhusu matumizi mabaya ya fedha katika Mkutano wa Smart Partnership.
Kwamba takribani shilingi bilioni nane zimefanyiwa ufisadi. Mdhibiti na Mkaguzi
Mkuu wa Hesabu za Serikali amenukuliwa akisema kwamba hajapat barua
yeyote inayomwomba (CAG haagizwi, anaombwa) kufanya ukaguzi maalumu
wa mkutano ule. Kamati ya Bunge ya PAC inaweza kutumia mamlaka yake
kumwomba CAG kufanya ukaguzi maalumu na kuwasilisha matokeo yake
kwenye Kamati na hatimaye Bungeni. Iliyokuwa Kamati ya POAC ilifanya wajibu
huu vizuri sana kwenye suala la nyumba ya Gavana wa Benki Kuu na kutokana
na ukaguzi huo hoja ile ilifungwa.
Ili kutekeleza wajibu huu muhimu wa uwajibikaji, Kamati za Bunge za mahesabu
ni lazima ziwezeshwe vya kutosha kwa mafunzo ya ujuzi (skills) na maarifa
(knowledge). Bila ya kuwa na uelewa mpana wa mambo Kamati hujikuta
zikifanya maamuzi ambayo yanakuwa na madhara makubwa kwa Taifa.
Katika kutekeleza wajibu, ni muhimu na lazima wajumbe wa Kamati kujiepusha
na vitendo vya rushwa kwani vitendo hivyo huzuia usimamizi na hatimaye
kuendeleza rushwa kwa wanaosimamiwa. Uwajibikaji ni silaha dhidi ya rushwa
na hivyo wanaosimaima uwajibikaji ni lazima wawe wasafi wao binafsi kwanza
kabla ya kusafisha walio wachafu. Uadilifu ni msingi muhimu sana katika
kujenga uwajibikaji. Bila ya uadilifu hakuna uwajibikaji na vile vile kukosekana
kwa uwajibikaji humomonyoa utamaduni wa uadilifu katika jamii.
Mambo gani ya kuzingatia?
Tumeona Wajibu wa Kamati katika kusimamia uwajibikaji wa Serikali.
Kiambatanisho kimeweka kinabaga ubaga majukumu na wajibu huo. Masuala
machache yafuatayo ni ya kuzingatia sana katika utekelezaji wa wajibu huu.
Moja, Pamoja na Matumizi yote ya Serikali ambayo Kamati husimamia,kuna
matumizi ambayo inabidi kuweka msisitizo maalumu. Moja ya matumizi hayo ni
ya Deni la Taifa. Katika Ripoti ya CAG ya mwaka 2012, hoja za kuhusu Deni la
Taifa zimeendelea kutokana na kasi ya ongezeko la Deni.
Kamati inapaswa
kufahamu kwamba Mzigo mkubwa wa Deni la Taifa ni katika kulipa ambapo
Fedha nyingi za umma hutumika. Kila mwaka Bajeti ya kuhudumia Deni la Taifa
huwa ni moja ya Bajeti kubwa zaidi ya Bajeti nyingine zote. Kwa mfano mwaka
2012/13, Serikali ilitenga takribani shilingi trilioni mbili kuhudumia Deni laTaifa
peke yake ilhali robo tu ya fedha hizo ilitengwa kwa ajili ya Wizara ya Afya.
Kamati zinapaswa kukagua kwa kina na kila wakati matumizi ya mikopo ili
kuhakikisha kwamba mikopo mingi inatumika kujenga uwezo wa nchi kuzalisha
rasilimali za kuhudumia mikopo hiyo kwa kukuza uchumi, kuzalisha ajira na
kuongeza kodi.
Pili, Makusanyo ya Kodi ya Serikali. Bunge hupitisha fedha kuwezesha Mamlaka
ya Mapato Tanzania kukusanya kodi. Hivi sasa ni takribani Watanzania milioni
moja tu ndio wanalipa kodi (kwa maana ya watu binafsi walio kwenye mfumo
rasmi). Hivyo tuna wigo mdogo sana wa kodi wakati tunatumia fedha nyingi
sana kukusanya kodi hiyo kidogo. Ni Wajibu wa Kamati kuona kwamba ufanisi
katika kukusanya kodi unafikiwa ikiwemo kwa kiasi kikubwa sana kuzuia mianya
ya ukwepaji wa kodi.
Kwa mujibu wa Mamlaka ya Mapato Tanzania, asilimia 15 ya makusanyo
tarajiwa huwa hayakusanywi kwenye idara ya Mapato peke yake kutokana na
ukwepaji wa Kodi. Hii ni sawa na takribani shilingi 490 bilioni kwa kutumia
makadirio ya mwaka wa fedha 2012/13. Wakati Bandari ya Dar es Salaam
inapakua makontena 600 kwa siku, kuna wakala wa upakuaji (clearingand
forwarding agents) wa idadi hiyo hiyo katika Bandari hiyo. Haiwezekani kuwe na
wastani wa kontena moja kwa kila wakala. Eneo hili linahitaji jicho pevu kutoka
kwenye Kamati za Bunge na Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali.
Ukwepaji kodi wa makampuni ya kimataifa pia ni ajenda kubwa ambayo kila
mara kamati inapaswa kuizingatia ili kuzuia.
Kamati ya PAC tayari imepitisha pendekezo la ukaguzi wa misamaha ya kodi
na kuiweka wazi (audit of tax exemptions and transparency). Ni matarajio
kwamba kwenye ripoti ya Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali kwa
mwaka unaoishia Juni 2013 Watanzania wataona taarfa ya ukaguzi wa
misamaha ya kodi.
Tatu, ukaguzi wa mikataba na taratibu za Manunuzi. Hili ni eneo ambalo
limekuwa chanzo kikubwa cha ubadhirifu katika nchi yetu. Ni muhimu kila mara
kamati kuzinagtia eneo hili katika kazi zake. Eneo hili linaathiri zaidi Mamlaka za
Serikali za Mitaa ambapo udokozi imekuwa kama utamaduni na hivyo
kuzorotesha utoaji wa huduma kwa wananchi. Ni muhimu Kamati kuhitaji mara
kwa mara ukaguzi maalumu kwenye manunuzi ili kujenga uwajibikaji katika
eneo hilo na kuepusha hasara kubwa kwa nchi.
Nne, hivi sasa nchi yetu imekuwa kitovu cha biashara ya dawa za kulevya.
Vijana wa kitanzania wamekuwa wakikamatwa maeneo mbalimbali duniani
wakihusishwa na biashara ya madawa ya kulevya. Moja ya njia ya kupambana
na uharamia huu ni uwajibikaji wa mamlaka zenye wajibu wa kupambana na
madawa ya kulevya. Hivyo, Kamati za Bunge zihoji katika mahesabu ya
mamlaka hizo matumizi ya fedha za umma kupambana na biashara ya
madawa ya kulevya ilhali biashara hiyo inazidi kushamiri. Iwapo tutawajibisha
Wizara ya mambo ya ndani kitengo cha kupambana na madawa ya kulevya
tutakuwa tumechangia katika vita hii. Hatuwezi kuwa tunatenga fedha kila
mwaka dhidi ya biashara hii haramu lakini bado inazidi kushamiri. Kila mwenye
wajibu awajibishwe.
Mwisho, Ukaguzi wa zoezi la ubinafsishaji. Bado sera ya ubinafshishaji
inatekelezwa na Serikali. Ni wajibu wa Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za
Serikali kukagua zoezi la ubinafsishaji na Kamati za Bunge kusimamia uwajibikaji
katika zoezi hili. Ubinafsishaji ni uuzaji wa mali ya Umma, hivyo ni lazima upate
usimamizi kamilifu.
Hitimisho
Kamati za Bunge za Mahesabu ni asasi muhimu za demokrasia kwani husimamia
uwajibikaji. Ni vema kamati hizi kupewa uzito stahili kwa kuwa na rasilimali za
kutosha katika kufanya kazi zake na kuhakikisha taarifa zake zinapata uzito
katika utekelezaji. Kimsingi Kamati zote za Bunge ni sawa kihadhi lakini Kamati za
mahesabu ndio Bunge kiuhalisia.
No comments :
Post a Comment