Mkurugenzi wa Kampuni ya kizalendo ya
Kotes (T) Ltd, Max Komba (wapili kulia-waliosimama), akikagua uchimbaji
mtaro kwa ajili ya kutandika nyanya za mfumo wa mawasiliano kwenye kituo
cha Polisi Oysterbay, Dar es Salaam, jana, kuunganisha kwenye mkongo wa
mawasiliano wa taifa. Kulia ni Mhandisi wa masuala ya ICT, Makao Makuu
ya Polisi, Mosses Maganza na watatu ni mhandisi wa Kotes (T) Ltd,
Mohamed Sibuga.
DAR ES SALAAM, Tanzania
JESHI la Polisi nchini limechukua hatua za kujiimarisha zaidi katika
kuukabili uhalifu kisasa zaidi kwa kuamua kuviunganisha vituo vyake
vikubwa kwenye mtandao wa mawasiliano katika mkongo wa taifa.
Kufuatia hatua hiyo, ujenzi wa miundombinu ya mawasiliano hayo ya
kuunganishwa kwenye mkongo wa taifa wa mawasiliano, umeshaanza kwenye
vituo vikubwa vya polisi katika mikoa ya Mwanza, Arusha, Kilimanjaro,
Zanzibar na jijini Dar es Salaam.
Akizungumza na waandishi wa habari jana, Mkurugenzi wa Kampuni ya
Kotes (T) Limited iliyopewa na jeshi la polisi kutengeneza miundombinu
hiyo, Max Komba, alisema, ujenzi huo ulianza kwenye Kituo cha Polisi
Kurasini, Chuo Cha Polisi Chang'ombe na Oysterbay ambako ujenzi wake
ulitarajiwa kukamilika jana.
Komba alisema, kampuni yake imepewa kufanya kazi katika mikoa hiyo
kwa wiki tatu, tangu ilipoanza Julai 27 mwaka huu kwa mujibu wa mkataba,
na ujenzi unatakiwa ume imekamilika ifikapo Agosti 20 mwaka huu.
Likizungumzia mradi huo, Jeshi la Polisi kupitia msemaji wake,
lilisema, mradi huo ukikamilika utasaidia jeshi hilo kupunguza gharama
na muda mwingi ambao limekuwa likilazimika kutumia katika kufuatilia
kumbukumbu katika kuwatambua wahalifu.
Msemaji wa Jeshi hilo, Advera Senso, alisema, kupitia mtandao huo,
vituo vilivyounganishwa vinaweza kupata taarifa na kuziona kwa wakati
mmoja na kwa haraka zaidi, jambo ambalo litawezesha kumbaini mhalifu
haraka zaidi na kuwa na ushahidi wa kutosha baada ya kumnasa.
"Mradi huu ni miongoni mwa maboresho mengi tunayofanya katika jeshi
la polisi ili kwenda na wakati. Hivyo baada ya kukamilisha kwenye vituo
vyenye hadhi ya mikoa kipolisi, tunatarajia pia kushuka hadi ngazi za
wilaya kulingana na mahitaji", alisema.
No comments :
Post a Comment