BAADA ya ukimya wa muda mrefu, mwimbaji nyota wa muziki wa kizazi kipya na dansi, Pauline Zongo ameibuka upya na kibao kipya kinachokwenda kwa jina la Misukosuko ya mapenzi.
Pauline amerekodi kibao hicho na kundi jipya la muziki linalojulikana kwa jina la Ndege Watatu, linaloundwa na wanamuziki wengine wawili wa kike, Khadija Mnoga na Joan Matovolwa.
Akizungumza mjini Dar es Salaam wiki hii, Pauline alisema tayari kibao hicho kimeshaanza kurushwa kwenye vituo mbalimbali vya redio nchini na kupokewa vizuri na mashabiki.
Mwanadada huyo, aliyekuwa mmoja wa wasanii wanaounda kundi la East Coast amesema, wameamua kuunda kundi hilo kwa lengo la kuleta changamoto mpya katika muziki.
Pauline alisema aliamua kuwa kimya kwa muda mrefu kwa sababu ya kulea mtoto wake wa pili mwenye umri wa mwaka mmoja na nusu. Mtoto wake wa kwanza ana umri wa miaka sita.
Alisema ukimya wake huo pia ulilenga kusoma mwelekeo wa muziki na pia kujipanga upya kabla ya kurudi ulingoni akiwa na vitu tofauti.
Mwanamama huyo, ambaye ni mwajiriwa wa bendi ya TOT Plus alisema, wameamua kuliita kundi lao kwa jina la Ndege Watatu kwa sababu sauti zao zinafanana na wanakijua wanachokifanya.
Pauline alisema uamuzi wake wa kujiunga na TOT Plus ulilenga kukuza kipaji chake cha muziki na pia kuwaonyesha mashabiki kwamba ana uwezo mkubwa katika fani hiyo.
"Kusema kweli, huwezi kuwa mwanamuziki kama hujui kupiga ala yoyote ya muziki,"alisema mwanamama huyo, ambaye ana uwezo wa kupiga gita, drums na kinanda.
Licha ya kundi lake la TOT kumruhusu kuwa mwanamuziki huru, Pauline alisema hawezi kutoa albamu kila mwaka kwa vile akifanya hivyo, hawezi kupata manufaa makubwa.
Alisema mwanamuziki anatakiwa kusonga mbele akiwa na mabadiliko badala ya kufanya kitu kile kile kila mwaka.
Mwanamama huyo alisema hakujifunza muziki kutoka kwa mtu yoyote. Anasema kuna siku alilala akaota ndoto anapiga gita, drums, kinanda na kuimba na alipozinduka usingizini, akaamua kutimiza ndoto yake hiyo.
Pauline anakiri kuwa, asili yake ni Jamhuri ya Kidemokrasi ya Congo. Anasema mama ni Mcongo na baba yake ni Mtanzania.
"Mimi nilizaliwa Congo. Wakati huo baba alikuwa akija Congo kibiashara ndipo akakutana na mama na kwetu tupo watoto wengi tu. Baadaye ikatokea kutokuelewana kati ya baba na mama, hivyo mimi na mdogo zangu tukaja Tanzania na baba na ndugu zangu wengine walibaki na mama Congo,"alisema.
Pauline anasema pia kuwa ni kweli kwamba anaye pacha wake wa kiume anayeitwa Paul Zongo, ambaye kwa sasa ni prodyuza wa muziki nchini Afrika Kusini. Alisema Paul ameshiriki kutengeneza nyimbo za kundi la Malaika la Afrika Kusini na wanamuziki wengine wa nchi hiyo.
Alipoulizwa iwapo ni kweli amezaa mtoto wake wa pili na mwigizaji filamu nyota wa Bongo, anayejulikana kwa jina la Mtunisi, alikiri kwamba ni kweli.
"Ndio ni kweli, lakini kwa sasa tumeshaachana, kila mtu ana maisha yake. Nina mchumba wangu, ambaye Mungu akitujalia, mwishoni mwa mwaka huu tutafunga pingu za maisha. Tumeshakaa kwenye uchumba kwa miaka miwili sasa.Mchumba wangu naye ni pacha kama mimi, tunapendana sana,"alisema.
Je, ni kitu kipi ambacho Pauline anakijutia katika maisha yake?
"Kiukweli sitaki kuficha, uhusiano nilioingia na baba mtoto wangu naujutia sana. Laiti ningesikiliza ushauri wa watu wengi, yasingenikuta yaliyonikuta,"alisema.
"Nilikuwa sisikilizi yote niliyokuwa naambiwa juu ya tabia za mwanaume huyo, lakini baada ya kuyaona, niliishia kujuta maana mapenzi yake yalinipotezea hata mwelekeo wa maisha yangu. Lakini kwa sasa nina nguvu mpya na nipo huru, nimejifunza siku nyingine sitafanya makosa,"alisisitiza.
Pauline alianzia muziki akiwa na kundi la East Coast lililokuwa na wasanii mahiri kama vile Crazy GK, Khamis Mwinjuma 'Mwana FA' na Ambwene Yesaya 'AY' kabla ya kuhamia TOT.
Akiwa East Coast, alijipatia umaarufu mkubwa aliposhiriki kuimba kibao cha Sister Sister akishirikiana na Crazy GK wakati akiwa TOT, aling'ara kupitia kibao cha Mnyonge Mnyongeni, alichokiimba kwa kushirikiana na Badi Bakule na Abdul Misambano.
No comments :
Post a Comment