Rais wa Shirikisho la Soka la Mali Hammadoun Kolado Cisse ametaka mabadiliko yafanyike ya mfumo wa upigaji kura kutafuta nchi itakayoandaa Kombe la Dunia.
Pia amesema bado hajaamua nani atampigia kura katika uchaguzi unaokuja wa Rais wa Fifa.
Kauli hiyo ameitoa licha ya Shirikisho la Soka barani Afrika kueleza litamuunga mkono Rais wa sasa wa Fifa Sepp Blatter na sio mpinzani wake pekee Mohamed Bin Hammam.
"Kwa wakati huu siwezi kuzungumzia mgombea gani tutakayemuunga mkono," alisema Cisse.
Katika mkutano uliofanyika mjini Cairo siku ya Jumatatu, Shirikisho la Soka barani Afrika, lilisema kamati yake kuu imekuwa na kura ya siri na imepitisha muswda wa kumuunga mkono Blatter katika uchaguzi wa Fifa.
"Kamati kuu inaweza kutoa mapendekezo, lakini chama au shirikisho la soka la nchi huamua kivyake nani wa kumpigia kura," Cisse alifafanua.
"Hawapaswi kufuata mapendekezo ya kamati na baadhi ya nchi zinamuunga mkono Blatter na nyingine bin Hammam.
"Tunataka mabadiliko ya kweli ndani ya Fifa - namna tunavyofanya kazi, jinsi usimamizi wa fedha ulivyo - lakini siwezi kusema iwapo hicho ndio kigezo cha kubadilisha Rais."
Cisse anataka Mkutano Mkuu wa Fifa kuliko wajumbe 24 wa kamati ya utendaji kutoa uamuzi wa mwisho ni nchi gani ya kuandaa Kombe la Dunia.
Mchakato huo umezongwa na tuhuma za rushwa.
"Iwapo kila nchi itaweza kupiga kura kwa nchi itakayoandaa Kombe la Dunia, hiyo itasaidia sana kupunguza tuhuma za rushwa kwa sababu huwezi kuhonga vyama na mashirikisho 203 ya soka."
Cisse ameongeza kundi la nchi za Afrika litashauri mabadiliko haya kabla ya uchaguzi haujafanyika tarehe 1 mwezi wa Juni, lakini akakataa kusema iwapo nchi nyingine zitaunga mkono.
Pia amesema angefurahi mfumo wa wajumbe wa Kamati Kuu ya Fifa nao ungeangaliwa na kuwa na wajumbe zaidi ya wanne wa sasa kutoka nchi za Afrika.
No comments :
Post a Comment