Azam FC leo hii majira ya saa nne asubuhi, imefanya mkutano maalum na waandishi wa habari klabuni kuzungumzia mambo mbalimbali yanayohusu klabu. mkutano wa leo umekuwa wa pili na waandishi wa habari tangia kuanza kwa msimu huu wa ligi 2009/2010
Ikumbukwe kuwa wiki chache kabla ya kuanza kwa ligi hii tulifanya mkutano kama huu ambapo pamoja na mambo mengine, tulimtambulisha nahodha wetu mpya Salum Swedi, na kuzungumzia mipango ya klabu katika ushiriki wetu ligi kuu.
Ushiriki wa Klabu ligi kuu
Mkutano wa leo, umekuja kufuatia kumalizika kwa raundi ya kwanza kwa mafanikio makubwa sana na klabu inatoa shukrani na heshma kubwa kwa wadau wote wa klabu ya Azam FC, hapa tunazungumzia mashabiki wetu, waandishi wa habari wote wa vyombo vyote vya habari, Viongozi wa mpira ngazi ya wilaya ya Ilala na mkoa wa Dar es Salaam, wachezaji na viongozi wa timu ambao kwa pamoja tumeiwezesha klabu yetu kwenda likizo ikiwa inashika nafasi ya pili.
Dhamira ya pili ya mkutano wa leo ilikuwa ni kuzungumzia mipango ya maendeleo ya klabu ya Azam FC pamoja na kujibu hoja na maswali kutoka kwa waandishi wa habari za michezo kutoka vyombo mbalimbali vya habari nchini.
Ujenzi wa uwanja na kituo cha michezo cha Azam FC,
Klabu ya Azam FC kupitia kwa makamu mwenyekiti wake mzee Said Mohammed imeweka bayana mipango ambayo inaendelea ya ujenzi wa uwanja na kituo bora cha mazoezi na makazi ya wachezaji katika eneo la Chamanzi wilaya ya Temeke. Kwa sasa eneo la ukubwa wa zaidi ya ekari 20 limeshapatikana na wataalamu wa usanifu na michoro toka nje ya nchi wanafanyia kazi kuweza kupata mchoro bora wa kiwango cha kimataifa utakaonendana matakwa ya mpira wa miguu na hadhi ya klabu ya ligi kuu.
Mafanikio makubwa kwa timu ya vijana
Mzee Said Mohammed amesema kama makamu mwenyekiti na kwa niaba ya bodi nzima ya wakurugenzi wa Azam FC anajivunia kuona ushiriki wa kiwango kikubwa kwa wachezaji wa timu ya vijana wa Azam FC Academy, ikumbukwe kuwa nyota wanaotamba sasa na Azam FC kama Mau Bofu Ally, Himid Mao Mkami, Awadh Mohammed na Tumba Swedi wamesajiriwa na kikosi cha Azam FC U-20.
Azam FC ndiyo klabu ya kwanza ya ligi kuu kuanzisha kikosi cha vijana bila kushurutishwa na mtu yoyote, na pia imekuwa timu ya kwanza kuweza kuwatumia vijana wa kikosi cha pili kwenye michezo ya ligi kuu kama tunavyoweza kuziona klabu kama Arsenal, Aston Villa, Liverpool na Manchester United zikifanya pale England
timu yetu ya vijana ndiyo mabingawa wanaoshikilia kombe la Uhai Cup kwa wachezaji wa umri chini ya miaka 20 kwa vilabu vya ligi kuu
Viongozi wa Kuajiriwa
Azam FC imekuwa klabu ya kwanza nchini kuwa na viongozi wa kuajiriwa na wakati shirikisho la mpira nchini lilipotangaza ulazima wa kuwa na Viongozi wa kuajiriwa, klabu ya Azam FC ilifanya kazi ya kupeleka tuu majina ya viongozi wake kwani tayari walikuwepo ofisini, haya pia ni mafanikio kwa klabu yetu ambayo tungependa kuyaweka wazi kwa Umaa.
Hakuna mchezaji yoyote wa kuachwa?
Kocha mkuu wa klabu ya Azam FC akichangia katika mkutano huo amesema kwa sasa kutokana na kiwango kizuri kwa kila mchezaji, hakuna mpango wa kumuondoa mchezaji yoyote. klabu itaendelea kuwa na wachezaji wote waliokuwepo kwenye raundi ya kwanza. Ikumbukwe kuwa Azam FC ndiyo timu inayoongoza nchini kwa kuwa na wachezaji wengi timu za Taifa ambapo Vladmir Niyonkuru (Burundi) Erasto Nyoni, Salum Swedi, Ibrahim Mwaipopo, Aggrey Morris, Himid Mao, na John Bocco (Taifa Stars) huku Selemani Kassim Selembe akichezea Zanzibar. utitiri huu wa wachezaji timu za taifa unaonesha ubora wa kikosi cha Azam FC.
Usajili
Klabu imetangaza kumsajiri kiungo kinda na nyota kutoka Mafunzo ya Zanzibar na timu ya taifa ya Zanzibar Selemani Kassim maarufu kama Selembe. Hadi sasa Selembe ndiye mchezaji pekee aliyesajiriwa na Azam FC kuongeza nguvu kwa ajili ya raundi ya pili inayotarajiwa kuanza Januari mwakani
Akijibu swali toka kwa mhariri wa Sports Extra Clouds FC Ibrahim Masoud Maestro, aliyetaka kujua siri ya mabadiliko ya ghafla ya kiuchezaji na morali wa wachezaji tangia Itamar Amorin achukue mikoba na Naider Dos Santos. Kocha mkuu wa Azam FC Itamar
Amorin amesema anadhani ni tofauti ya mawasiliano pekee, Itamar amesema mtangulizi wake ambaye ni Mbrazil mwenzake alikuwa kocha mzuri sana lakini wakati mwingine matokeo hayaletwi na ubora wa mbinu za kocha pekee bali hata mfumo, mawasiliano, bahati na wakati.
Kuhusu wachezaji wa Kigeni
kiwango kilichooneshwa na wachezaji watanzania kimekuwa kikubwa sana kuliko wachezaji wa kigeni, Wachezaji watanzania wamebadilika sana, wamecheza kwa bidii na maarifa makubwa sana katika raundi ya kwanza kuliko wageni. na hili unaweza kuliona katika orodha ya wafungaji bora ambapo licha ya ligi kuu kuwa na lundo la washambuliaji wa kigeni lakini orodha hii inashikwa na watanzania wakiongozwa na John Bocco Adebayor wa Azam FC aliyemaliza raundi ya kwanza akiwa na magoli tisa
Kujitoa kombe la Tusker
Kumekuwa na minong’ono isiyo rasmi juu ya uamuzi wa Azam FC kujitoa kwenye michuano ya Tusker Challenge Cup ambapo Makamu Mwenyekiti Mzee Said Mohammed ameona umuhimu wa kulitolea ufafanuzi
Ukweli ni kwamba Azam FC haikujitoa kwa sababu michuano hii inadhaminiwa na kinywaji bali ni kutokana na sababu za kitaalam na kiungozi zaidi.
Kwanza Azam FC ina wachezaji Tisa kwenye timu za Taifa ambazo zinajiandaa na michuano ya Challenge Cup na katika timu yenye wachezaji 24, unapoondoa wachezaji tisa unaiacha na wachezaji 15 ambapo kati yao kuna wachezaji wa kigeni kama Ibrahim Shikanda ambao wakiondoka timu inabaki na wachezaji ambao hawatoshi kujiandaa vema na ushiriki wa michezo hii.
Wachezaji wa Azam FC waliopo timu za Taifa zinazojiandaa na Challenge Cup ni Vladmir Niyonkuru (Burundi) Erasto Nyoni, Salum Swedi, Ibrahim Mwaipopo, Himid Mao, na John Bocco (Kilimanjaro Stars) huku Selemani Kassim Selembe na Aggrey Morris, wakichezea Zanzibar
Pia Azam FC ni klabu inayoendeshwa kwa kufuata misingi ya uweledi (professionalism), tulikwisha jiwekea ratiba yetu (calendar) ambapo ratiba ya klabu ilikuwa ikionesha mapumziko kwa wachezaji wakati raundi ya kwanza itakapo malizika, endapo utawarudisha wachezaji kambini hasa wale wa kigeni utalazimika kuwalipa, kuharibu ratiba ya mwalimu, na kupoteza pesa za nauli kwenye mashirika ya usafiri ambako tulifanya booking. Azam FC iliomba kujitoa kutokana na taarifa ya ushiriki wetu kutufikia kuwa ya mmno na kwa bahati nzuri TFF walikubaliana na ombi letu alisema.