Afisa
michezo wa Jiji la Mbeya, Joyce Mwakifwamba(kulia) akimkabidhi jezi
mmoja ya wachezaji wa mchezo wa Pool Mkoani Mbeya wakati wa kukabidhi
vifaa vya michezo kwa vilabu shiriki vya mashindano ya Safari Pool taifa
ngazi ya Mkoa.
WADAU
wa mchezo wa Pool wametakiwa kuandaa viwanja vingine vya mchezo huo nje
ya kumbi za baa ili kutoa fursa ya watoto kujifunza na kuuelewa mchezo
huo.
Wito
huo umetolewa na jana na Afisa michezo wa Jiji la Mbeya, Joyce
Mwakifwamba wakati akikabidhi vifaa vya mchezo huo kwa ajili ya
mashindano maalum ya kukuza mchezo huo mkoani hapa ambayo yamedhaminiwa
na Kampuni ya Bia Tanzania (TBL).
Mwakifwamba
alisema kuwa licha ya mchezo wa pool hivi sasa unawapenzi wengi na
umeendelea kujizolea umaarufa katika maeneo mengi nchini, viwanja vingi
vya mchezo huo vipo kwenye kumbi za mabaa, hivyo sio vema watoto
wakashirikishwa ili kulinda maadili ya taifa.
Alisema
kuwa ili kuibua vipaji na kuendeleza mchezo huo kwa vijana wadogo, ni
busara kuanza kuandaa viwanja vingine nje ya kumbi za mabaa kwa ajili ya
matumizi ya vijana na watoto.
“Mchezo
wa Pool umeanza kuwa maarufu nchini na kwa muda mfupi umejizolea
wapenzi wengi, lakini changamoto kubwa iliyopo ni viwanja vingi kuwa
ndani ya mabaa, natoa wito kwa wadau wa mchezo huu kuandaa viwanja vya
watoto ili kuendeleza mchezo huu,” alisema Mwakifwamba.
Mashindano
hayo yaliyoanza kutimua vumbi Septemba 6 mwaka huu yanatarajia kufikia
kilele chake Septemba 10, mwaka huu katika ukumbi Blue House eneo la
Kabwe Jijini Mbeya yakishirikisha timu tisa kutoka wilaya mbalimbali za
mkoa wa Mbeya.
Pia
Mwakifwamba alizitaka timu zinazoshiriki mchezo huo kuwa na nidhamu ya
hali ya juu na kukubali matokeo hata pale zinapokuwa zimeshindwa na
wapinzani wao.
Meneja
matukio wa TBL Kanda ya Nyanda za Juu Kusini, Francis Mwasamwene,
alisema kuwa lengo la TBL kudhamini mashindano hayo ni kuibua vipaji vya
wachezaji wa mchezo huo mkoani Mbeya, na kuviendeleza.
Mwasamwene
alitoa wito kwa wachezaji wengi zaidi wenye mapenzi na mchezo huo
kujitokeza kushiriki mashindano hayo kwa kuwa hadi sasa kuna jumla ya
timu tisa tu zinazojulikana mkoani Mbeya.
“Tunahitaji
kuona mchezo huu ukiwa na timu nyingi zaidi mkoani hapa na hili
litafanikiwa zaidi kwa timu nyingi zaidi kujisajili, TBL imeamua
kudhamini mashindano haya ili kuweza kuibua vipaji vya wachezaji wa
mchezo huu,”.
Kwa
upande wake Mwenyekiti wa mchezo wa Pool mkoani Mbeya, Obeidy Malabeja,
alisema mchezo huo ni kama ilivyo michezo mingine na unaendeshwa kwa
sheria zake halali zinazoulinda.
Malabeja
alizitaja timu zitakazoshiriki mashindano hayo kuwa ni Container ya
Tunduma wilayani Momba, Nakonde, Lunch Time ya Mbozi, Kizota, Royal
Zambezi, Blue House, Shooters, Royal Class na Stendi Kuu ya mabasi
mkoani Mbeya.
Vifaa
vilivyotolewa na TBL na kukabidhiwa kwa timu hizo na Afisa Michezo wa
Jiji la Mbeya, Joyce Mwakifwamba ni pamoja na Jezi seti moja pamoja na
simu ya mkononi kwa kila timu inayoshiriki mashindano hayo.
No comments :
Post a Comment