Michoro ya ujenzi wa Kampasi ya
Mloganzila iliyo kijijini Kwembe katikati ya Wilaya za Kisarawe Mkoa wa Pwani
na Kinondoni Mkoa wa Dar es salaam. Hii ni sehemu ya Chuo cha Afya na Sayansi
Shirikishi Muhimbili
(MUHAS) inayojengwa kwenye eneo la
ekari 3800 kwa ajili ya kutolea mafunzo kwa wanafunzi wa udaktari na huduma za
Afya wapatao 15,000 kwa mwaka, na pia itakua sehemu ya kutolea matibabu ya
maradhi yote makuu na ya kawaida nchini.
Kwa mujibu wa Makamu Mkuu wa Chuo
cha Afya na Sayansi Shirikishi Muhimbili, ujenzi wa Hospitali hii, ambayo pesa
ya ujenzi wake imeshapatikana, unatarajiwa kuanza mwishoni mwa mwezi Januari,
2013 na unatarajiwa kukamilika miaka miwili baada ya ujenzi kuanza. Kwa maneno
mengine Kampasi ya Muhimbili ya Mloganzila inategemewa kuanza kazi mwanzoni mwa
mwaka 2015.
Tayari wataalamu na wafanyakazi
wanaotarajiwa kufanya kazi katika kampasi ya Mloganzila wameshaanza mafunzo
ndani na nje ya nchi. Mara hospitali hiyo kubwa na ya kisasa itakapokamilika
itakua na uwezo wa vitanda vya kulaza wagonjwa mia sita (600).
Sambamba na kampasi ya MUHAS ya Mloganzila pia ujenzi wa
Kampasi ya Afya ya Chuo Kikuu cha Dodoma (UDOM) umeshaanza na kufikia hatua ya
juu na ambapo pia hospitali hiyo inatarajiwa kuanza shughuli zake rasmi mwaka
2015.
Kwa mujibu wa Mkurugenzi wa Mfuko wa Afya ya Jamii
(National Health Insurance Fund) NHIF Bw. Emmanuel Humba mchakato wa
kufanikisha uanzishaji wa Chuo Hospitali hiyo vimeshaanza ambapo baadhi ya
wataalamu wakiwemo Madaktari na watumishi wengine wako nchini na nje ya nchi
kwa ajili ya masomo na mafunzo mbalimbali.
Chuo hicho kinatarajia kuwa na vifaa vya kisasa vya tiba
vinavyokidhi mahitaji ya Afya na Elimu ya Udaktari wa kiwango cha Kimataifa,
ikiwa ni mikakati kabambe ya serikali ya awamu ya nne katika
kuhakikisha nchi ina wataalamu wengi na huduma za kisasa za afya ili kuondokana
na adha ya kupeleka wagonjwa nje ya nchi kwa ajili ya matibabu.
Kwa sasa MUHAS inachukua takriban wanafunzi 2442 wa udaktari na huduma za afya kwa mwaka. Hivyo ujio wa kampasi ya Afya Mloganzila na Kampasi ya afya ya UDOM utaharakisha mpango wa serikali wa kupunguza wastani wa wagonjwa kwa daktari mmoja kwa kiwango kikubwa. Hivi sasa wastani ni daktari mmoja anahudumia wagonjwa 30,000.
No comments :
Post a Comment