Mpiga Picha Mkuu wa Kampuni ya Free Media inayochapisha magazeti ya
Sayari na Tanzania daima, Joseph Senga (kushoto) akiangalia aina mpya ya
Samsung Galaxy Camera wakati wa uzinduzi wa camera hiyo jijini Dar es
Salaam.
Na Mwandishi Wetu
KAMPUNI ya Samsung Tanzania, juzi usiku imezindua rasmi
bidhaa mpya ya Samsung Galaxy Camera, ambapo kwa kushirikiana na Kampuni ya
Simu ya Vodacom wameweka kifurushi cha 1GB kwa muda wa miezi mitatu.
Akizungumza katika hafla ya uzinduzi huo kwenye Hoteli ya
Serena jijini Dar es Salaam juzi, Meneja Mkuu wa Samsung Tanzania, Kishor
Kumar, alisema kuwa, Samsung Galaxy Camera ni zaidi ya simu yenye kamera
kiutendaji na ubora wa huduma zake.
Aliongeza kuwa, Samsung Galaxy Camera, ina CMO sensor,
ambayo inawezesha kamera hiyo kuchukua picha zenye ubora wa hali ya juu.
Katika uzinduzi huo wa Galaxy Camera, ambayo ni ya kisasa
zaidi, Minhai Patel aliibuka na zawadi ya aina hiyo mpya ya kamera katika droo
ndogo iliyoshirikisha waalikwa waliohudhuria uzinduzi.
Kwa upande wake, Meneja Usambazaji na Mauzo wa Samsung
Mobile, Sylvester Manyara, alisema kuwa, Galaxy Camera ina tofauti na kamera
nyingine, kwa sababu yenyewe inatumia mtandao wa 3G, unaoiwezesha kupata huduma
ya Internet ya kasi.
Aliongeza kuwa, Galaxy Camera ina uwezo wa kutuma picha hadi
katika mitandao ya kijamii ya Facebook, Twitter, Whatsapp na Instagram na
kwamba kamera hizo zinatoa picha za ubora zaidi hata zilizopigwa kutoka umbali
mrefu.
No comments :
Post a Comment