SHIRIKISHO la Kimataifa la Vyama vya Mpira wa Miguu (FIFA) limesema
litaifungia Tanzania iwapo itabainika kuwa Serikali imekuwa ikiingilia shughuli
za Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF).
FIFA
imesema kumekuwa na shutuma kupitia taarifa mbalimbali za vyombo vya habari
nchini kuwa Wizara ya Habari, Vijana, Utamaduni na Michezo imeonesha nia ya
kuingilia uendeshaji wa TFF.
Kwa
mujibu wa barua ya jana (Machi 10 mwaka huu) ya FIFA kwenda kwa Rais wa TFF,
Leodegar Tenga, vyombo vya habari vimemkariri Waziri (Dk. Fenella Mukangara)
kuwa Serikali imeiagiza TFF kutumia Katiba ya mwaka 2006 katika uchaguzi wakati
tayari imeshafanyiwa marekebisho.
“Pia
imeelezwa kuwa TFF imetakiwa kufanya Mkutano Mkuu pamoja na ule wa uchaguzi kwa
tarehe ambazo zimepangwa na Serikali. Vilevile imeelezwa kuwa Serikali
inakusudia kuunda Kamati ya Muda iwapo TFF haitatekeleza maagizo yake,” imesema
sehemu ya barua hiyo iliyosainiwa na Katibu Mkuu wa FIFA, Jerome
Valke.
FIFA
imesema iwapo yaliyoripotiwa na vyombo vya habari yatathibitika kuwa kweli,
maana yake huo ni uingiliaji wa wazi wa Serikali kwa shughuli za
TFF.
“Tunapenda kuwakumbusha kuwa wanachama wote wa FIFA wanatakiwa
kuendesha shughuli zao kwa uhuru bila kuingiliwa na mtu mwingine kama
ilivyoelezwa katika ibara za 13 na 17 za Katiba ya FIFA.
“Hivyo
kama maagizo hayo yanayodaiwa kutolewa na Serikali yatatekelezwa, suala hili
litapelekwa katika mamlaka za juu za FIFA kwa hatua zaidi ikiwemo kuisimamisha
Tanzania kama ambavyo inakuwa pale panapokuwa na uingiliaji wa Serikali,”
imesema barua hiyo.
Barua
hiyo ambayo nakala yake pia imetumwa Shirikisho la Mpira wa Miguu Afrika (CAF)
imeelezea baadhi ya athari ambazo Tanzania itakumbana nazo endapo itasimamishwa
ni timu za taifa pamoja na klabu kutoshiriki mechi za kimataifa kwa mujibu wa
Ibara ya 14 ya Katiba ya FIFA.
Vilevile si TFF au wanachama wake na maofisa wengine watakaoweza
kunufaika na programu za maendeleo, kozi au mafunzo yanayotolewa na FIFA na
CAF.
“Madai
ya uamuzi uliofanywa na Wizara ya Habari, Vijana, Utamaduni na Michezo ni ya
kusikitisha kutokana na ukweli kuwa FIFA ilishatangaza itatuma ujumbe wake
kuchunguza jinsi hali ilivyo kwa sasa na kutoa mapendekezo yake. Kutokana na
hali hii, ujumbe wa FIFA uliokuwa uje kuchunguza (suala la uchaguzi) itabidi
usubiri kwa vile ni muhimu kushughulikia tatizo hili kwanza.
“Katika
mazingira haya tunaomba ueleze msimamo huu wa FIFA kwa mamlaka zinazohusika
(Serikali) na athari ambazo mpira wa miguu wa Tanzania utakumbana nazo.
Tunakushuru na tunatarajia utatufahamisha kila hatua inayoendelea katika suala
hili,” imesema barua hiyo.
Boniface
Wambura
Ofisa
Habari
Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF)
No comments :
Post a Comment