TAARIFA KWA VYOMBO VYA HABARI
19/03/2010Jumatatu tarehe 15/03/2010 wakati wa mchezo wa Ligi Kuu ya Vodacom kati ya Yanga na Moro United uliofanyika uwanja wa Uhuru Dar es Salaam, mmoja wa wauza tiketi, Mohamed Baruani alikutwa na kitabu kimoja cha tiketi ambacho hakikuwa miongoni mwa vitabu vilivyokabidhiwa rasmi kwa wauzaji wa tiketi.Wakati akihojiwa muuzaji huyo alisema alikabidhiwa kitabu hicho cha tiketi na mmoja wa maofisa wa TFF wanaohusika na masuala ya tiketi.
Kutokana na hali hiyo maofisa wa Polisi waliendelea kufuatilia ikiwemo kuwahoji wahusika.
Miongoni mwa hao waliohojiwa na kwa maana hiyo wanalisaidia jeshi la polisi, ni afisa wa TFF Daniel Msangi pamoja na baadhi ya watendaji wa kiwanda cha Inter Press of Tanzania Limited, ambao ni wachapishaji wa tiketi za mchezo kati ya Yanga na Moro United.
Kwa mantiki hiyo suala hili lipo mikononi mwa Polisi na linashughulikiwa kwa mujibu wa taratibu za kisheria.
TFF inashukuru na kuwapongeza wale wote waliotoa taarifa ambazo baadaye zilifanikisha kubainika uwepo wa kitabu kilicho nje ya utaratibu na inaahidi kwa dhati kuwa itatoa kila aina ya ushirikiano kwa jeshi la Polisi katika kushughulikia jambo hili.
Kwa kuwa tukio hili bado limo mikononi mwa Polisi na linafanyiwa kazi kwa utaratibu wa kisheria ni vema TFF, wadau wa mpira na jamii kwa jumla kuwa na subira na kuicha dola kufanya kazi yake.
TFF inachukia vitendo vyovyote vinavyosababisha kuvuja kwa mapato yatokanayo na viingilio vya mpira wa miguu na inayo nia ya dhati ya kuhakikisha fedha zinazopatikana kwenye mpira zinausaidia mpira wenyewe.
Katika kutekeleza hilo TFF iliunda Kamati maalumu ambayo pamoja na mambo mengine ni kazi yake ni kukusanya maoni ya wadau ili kubaini na hatimaye kuziba mianya ya upotevu wa fedha zitokanazo na mapato ya viingilio.
Fredrick Mwakalebela
KATIBU MKUU
No comments :
Post a Comment