LONDON, England
“Tayari
tulishapata wa kujaza nafasi ya Van Persie kabla ya kumruhusu na kusema
kweli sitarajii kusajili yeyote wa kumrithi, ninao wengi kikosini.”
KOCHA
Arsene Wenger wa Arsenal, amekiri kusikitishwa na maamuzi magumu
aliyochukua ya kumuuza Robin van Persie kwa mahasimu wao Manchester
United, ingawa amesema hatomsajili mbadala wake, kwani tayari alishapata
kabla ya kumruhusu.
Akizungumza na vyombo
vya habari baada ya kukubaliana ada ya uhamisho na United, Wenger
alisema: “Ni huzuni kubwa unapopoteza mchezaji wako bora kama yeye.
Alibakisha mwaka mmoja kwenye mkataba wake, hivyo hatukuwa na chaguo
zaidi.”
Alipoulizwa
kama atatumia kiasi cha pesa alichovuna kumuuza mkali huyo kusajili
wachezaji wapya, Wenger alijibu: “Tayari tulishapata wa kujaza nafasi
yake kabla ya kumruhusu na sitarajii kusajili yeyote wa kumrithi, ninao
kikosini.”
Katika taarifa ya klabu kwenye
tovuti, Gunners ilisema: “Van Persie atasafiri kwenda Manchester leo
Alhamisi, kwa ajili ya makubaliano binafsi, ikiwamo vipimo vya afya ili
kumalizia hatua zilizosalia za uhamisho wake.”
Kwa
upande wake Msemaji wa United aliongeza: “Tuna furaha kutangaza kuwa,
tumekubaliana na Arsenal kwa ajili ya uhamisho wa Robin Van Persie kuja
Man United.”
Aidha kocha Sir Alex Ferguson,
ametambia usajili wa Van Persie ulioigharimu klabu yake pauni milioni
22, huku nyota huyo akiahidi ushambuliaji pacha tishio utakaobeba tija
na nyota wa Manchester United, Wayne Rooney.
Van
Persie aliyekuwa nahodha wa Arsenal, jana alikuwa Old Trafford yaliko
makazi ya Man United, kwa ajili ya vipimo vya afya yake, ikiwamo
makubaliano binafsi ya mshahara wake unaotarajiwa kuwa zaidi ya pauni
200,000 kwa wiki.
Taarifa za kukubali kwa
Gunners kumruhusu Mholanzi huyo kujiunga na United zilitolewa juzi,
ambapo Fergie alisema ana matumaini makubwa ya kumaliza kila kitu kuhusu
mkali huyo kufikia wikiendi hii.
Van Persie, 29, ambaye alikataa kurefusha mkataba wake na Arsenal,
alimwambia kocha huyo Mskochi kuwa yu tayari kutumika kama pacha wa
mbele au nyuma ya Rooney na kwamba atakuwa na ushirika mwema.
Kukubaliwa
kwa dau la United kupata saini ya RVP kulipokelewa kwa furaha na
Rooney, aliyeingia kwenye kurasa ya ‘twitter’ na kumtania shabiki
maarufu wa Arsenal aitwaye Piers Morgan.
Akaandika
kwenye ukurasa huo: “Arrrr, maskini Piers. Uhalia gani kwa sasa,
mkubwa?”, ambapo bila kusita Morgan akaujibu ujumbe huo kwa kumuita
Rooney “mshambuliaji namba mbili klabuni Old Trafford.”
No comments :
Post a Comment