Mabeki wa
Taifa Stars, wakimwangilia mshambuliaji wa Botswana ‘Zebras’ akifunga
bao la tatu, wakati wa mechi ya kirafiki iliyochezwa kwenye uwanja wa
Molepolole mjini Gaborone, jana.
Mshambuliaji wa Taifa Stars Mrisho Ngassa akijaribu kumtoka beki wa timu ya Botswana,
‘Zebras’ Oscar Neenga wakati wa mechi ya kirafiki ya Kimataifa
iliyochezwa kwenye Uwanja wa Molopolole mjini Gaborone Bostwana juzi na
kumalizika kwa sare ya mabao 3-3.
Mshambuliaji wa Taifa Stars Mrisho Ngassa akijaribu kumtoka beki wa timu ya Botswana,
‘Zebras’ Oscar Neenga wakati wa mechi ya kirafiki ya Kimataifa
iliyochezwa kwenye Uwanja wa Molopolole mjini Gaborone Bostwana juzi na
kumalizika kwa sare ya mabao 3-3.
Taifa
Stars imetoka sare ya mabao 3-3 na wenyeji Botswana (Zebras) katika
moja kati ya mechi kadhaa za kirafiki za kalenda ya Shirikisho la
Kimataifa la Mpira wa Miguu (FIFA) zilizochezwa leo (Agosti 15 mwaka
huu) usiku.
Hadi
mapumziko kwenye mechi hiyo iliyochezwa Uwanja wa Molepolole ulioko
Kilometa 40 nje ya Jiji la Gaborone, timu hizo zilikuwa zimefungana
mabao 2-2. Stars ndiyo iliyokuwa ya kwanza kupata bao dakika ya 17
lililofungwa kwa penalti na beki Erasto Nyoni.
Mwamuzi
Lekgotia Johannes Stars alitoa adhabu hiyo baada ya beki Oscar Obuile
Ncenga wa Zebras kumuangusha ndani ya eneo la hatari mshambuliaji Mrisho
Ngasa aliyekuwa akimkabili kipa Mompoloki Sephekolo.
Bao
hilo halikudumu muda mrefu, kwani Zebras walisawazisha dakika ya 26
baada ya shuti kali lililopigwa na Lemponye Tshireletso nje ya eneo la
hatari kumshinda nahodha wa Taifa Stars, Juma Kaseja. Dakika tano
baadaye kiungo mshambuliaji Mwinyi Kazimoto aliifungia Stars bao la pili
kwa shuti la mbali.
Tshireletso
aliisawazishia tena Zebras dakika ya 37. Mfungaji alifunga bao hilo kwa
kichwa akiunganisha mpira wa krosi kutoka wingi ya kushoto uliopigwa na
Tebogo Sembowa ambaye kabla alimtoka beki Aggrey Morris.
Kipindi
cha pili kilianza kwa Kocha Kim Poulsen wa Stars kuwatoa Frank Domayo
na Salum Abubakar na nafasi zao kuchukuliwa na Shabani Nditi na Athuman
Idd.
Safari
hii Zebras ndiyo walioanza kufunga dakika ya 69 ambapo kiungo Michael
Mogaladi aliifungia bao la tatu kwa kichwa akiunganisha krosi fupi
iliyotokana na mpira wa kurusha.
Dakika
13 za mwisho Stars walicheza pungufu baada ya beki Erasto Nyoni
kutolewa nje kwa kadi nyekundu kutokana na kumchezea rafu mshambuliaji
Lovemore Murirwa.
Mrisho
Ngasa ambaye alikuwa nyota kwenye mchezo huo aliisawazishia Stars
dakika ya 84 baada ya kugongeana one-two na mshambuliaji Simon Msuva
aliyetokea benchi kuchukua nafasi ya Haruna Moshi.
"Licha
ya timu kucheza vizuri, tatizo kubwa lilikuwa kwenye safu ya ulinzi
ambapo mabeki waliruhusu mipira mingi ya krosi na kuwaacha washambuliaji
wa Botswana wakifunga bila bughudha. Mabeki hawatakiwi kuruhusu mipira
ya krosi, wakiruhusu ni lazima wahakikishe wanawadhibiti washambuliaji
wa timu pinzani.
"Kwa
upande wa washambuliaji, Said Bahanuzi alikuwa akicheza mechi yake ya
kwanza ya kimataifa akiwa na Stars tangu nilipomjumuisha kwenye timu kwa
mara ya kwanza.
Kuna makosa madogo madogo ambayo niliyatarajia, hivyo nitamrekebisha polepole," alisema Kocha Poulsen mara baada ya mechi hiyo.
Stars;
Juma Kaseja, Erasto Nyoni, Amir Maftah, Aggrey Morris, Kelvin Yondani,
Frank Domayo/Shabani Nditi, Mrisho Ngasa, Salum Abubakar/Athuman Idd,
Said Bahanuzi/Simon Msuva, Haruna Moshi/Ramadhan Singano na Mwinyi
Kazimoto.
Zebras;
Mompoloki Sephekolo, Tshepo Motlhabankwe/Tshepo Maikano, Edwin Olerile,
Oscar Obuile Ncenganye, Mompati Thuma, Patrick Motsepe/Jackie
Mothatego, Lemponye Tshireletso, Michael Mogaladi, Tebogo Sembowa,
Ntesang Simanyana na Galabgwe Moyana/Lovemore Murirwa.
Stars
inayodhaminiwa na Kilimanjaro Premium Lager inarejea nyumbani kesho
(Agosti 16 mwaka huu) ambapo itawasili Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa
Julius Nyerere (JNIA) saa 1.20 usiku kwa ndege ya Kenya Airways.
No comments :
Post a Comment