MAMIA ya wadau wa michezo nchini, wamejitokeza kuuaga mwili wa marehemu, Meneja wa Uwanja wa Taifa na Uhuru, Charles Massanja (52) aliyefariki dunia usiku wa kuamkia Jumatatu nyumbani kwake Kimara, Dar es Salaam baada ya kuangukiwa na ukuta wa nyumba yake.
Katika kuuaga mwili wa marehemu Massanja, siku ya Jumanne, viongozi mbalimbali wa serikali, Vyama vya Michezo, viongozi wa Klabu mbalimbali na wadau wengine walihudhiria, ambapo mwili wake unatarajiwa kusafirishwa kesho kwenda nyumbani kwao Urambo, Tabora kwa maziko.
Akiongoza mamia ya waombolezaji katika maombolezo yaliyofanyika Uwanja wa Uhuru, Dar es Salaam, Naibu Waziri wa Habari, Utamaduni na Michezo, Joel Bendera alizungumza kwa niaba ya serikali na kusema Massanja alikuwa ni kiongozi mwenye nidhamu asiyependa makuu.
Amesema kifo chake cha gafla kimewashtua wadau wengi wa michezo na pengo aliloacha halitaweza kuzibika kwani alikuwa ni miongoni mwa wataalam wachache katika michezo hapa nchini.(NAIBU WAZIRI WA HABARI UTAMADUNI NA MICHEZO JOEL BENDERA AKIWEKA SHADA LA MAUA KATIKA JENEZA LA MASANJA)Amesema ninautambua uwezo wa Massanja tangu zamani ila Mwenyezi Mungu amempenda zaidi ndio maana amemchukua, hivyo hatuna budi kumuombea kwa mungu ailaze roho yake mahala pema peponi, amina.
Naye Mkurugenzi wa Maendeleo ya Michezo nchini, Leonard Thadeo amemzungumzia Massanja kwa kusema, alikuwa anajali kazi yake kwa kuipenda ambapo alikuwa akiitumikia bila kusukumwa na mtu ndicho kitu kilichosababisha kupendwa na wadau wa michezo.
Mbunge wa Ilala, Idd Azan naye alikuwepo katika kuuaga mwili wa Massanja ambapo amesema mpaka sasa hawajui ni nani atakayeweza kuziba pengo lililoachwa na Massanja kwani alikuwa mtu wa watu, itachukua muda kusahau mazuri yake.
Amesema wadau wa michezo hawana budi kumuombea kwa mungu aepukane na adhabu ya kaburi, kwa jinsi alivyokuwa akijitolea kwa wanamichezo mbalimbali hawana budi kumshukuru.
Pia Mwenyekiti wa Baraza la Michezo la Taifa, Idd Kipingu amemzungumzia Massanja kwa kusema, marehemu alikuwa akifanya kazi katika eneo nyeti na aliweza kulimudu bila matatizo yoyote kwa kuweza kushirikiana na watu vizuri bila malalamiko ya hapa na pale.
Amewaomba viongozi wa Vyama vya michezo wamuenzi Massanja kwa kuiga yale mazuri ambayo alikuwa akiyafanya likiwemo la nidhamu ambapo ndicho kitu kilichomfanya akubalike miongoni mwa wadau wa michezo.
Naye Rais wa Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF), Leodgar Tenga amesema, wao ndio wadau wakubwa wa soka hapa nchini wamesikitishwa na kifo hicho cha gafla kwani alijitolea maisha yake katika soka na huwezi kuzungumzia maendeleo ya soka bila kulitaja jina lake.(Bi. Devotha, mke wa marehemu akiaga mwili wa mumewe kwenye uwanja huo)Nao Wenyeviti wa Klabu kongwe nchini za Simba na Yanga kwa nyakati tofauti walimzungumzia Massanja ambapo Hassan Dalali wa Simba amesema siku ya mchezo wa timu yao dhidi ya JKT Ruvu alitaniana na marehemu kwa kubishana kwamba marehemu alitaka Dalali akakae kwenye jukwaa kuu na Dalali alikataa kwa kusema huko wanakaa viongozi wa serikali tu.
Naye Iman Madega wa Yanga, amesema wamempoteza mwanachama wao hai kwani alikuwa akiwasaidia mambo mengi uwanjani na pia alifundisha soka timu mbalimbali hapa nchini.
Massanja alizaliwa miaka 52 iliyopita huko Urambo, Mkoani Tabora na kupata elimu ya sekondari katika shule za Itaga mjini Tabora na Minaki jijini Dar es Salaam kuanzia mwaka 1972 mpaka 1977 na baadaye kuendelea na elimu ya juu kwa kupata Shahada ya Uzamili wa Physical Education nchini Cuba mwaka 1988.
Enzi za uhai wake Massanja aliwahi kufanya kazi na miaka yake katika mabano za Ofisa Michezo Daraja la Kwanza(2007), Meneja wa Uwanja wa Taifa na Uhuru (2006 mpaka umauti unamkuta), Katibu Mkuu Msaidiu wa Chama cha Mpira wa Miguu Tanzania enzi hizo kikijulikana FAT (1995-96, 2002-04), Ofisa Michezo Idara ya Mendeleo na Michezo(1996-2001) na Kocha Mkuu wa timu ya African Sports ya Tanga (1990-1994).
Mungu ailaze roho ya marehemu mahala pema peponi. Amina
FEAJ KUTETEA HAKI ZA WAANDISHI
-
*Mwandishi wetu,Kigali*
Shirikisho jipya la Waandishi wa habari Afrika Mashariki(FEAJ) limeanzishwa
ili kusaidia kutetea haki na maslahi ya wafanyakazi ...
10 hours ago
No comments :
Post a Comment