Na Mwandishi Wetu
UCHAGUZI wa Chama cha Netiboli Mkoa wa Dar
es Salaam (CHANEDA) uliokuwa ufanyike leo, sasa umeahirishwa hadi Agosti
17, mwaka huu.
Akizungumza na gazeti hili jijini Dar es
Salaam jana, Ofisa Michezo wa Ofisi ya Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam,
Adolf Halii, alisema kuwa kuahirishwa kwa uchaguzi huo kunatokana na
ukumbi uliopangwa kufanyika tukio hilo kuwa na shughuli nyingine.
Alisema kuwa maandalizi yote ya uchaguzi
huo, ikiwa ni pamoja na usaili, yalishakamilika, lakini ukumbi
waliopanga kuutumia wa ofisi ya Mkuu wa Mkoa, utatumika kwa shughuli
nyingine ya ghafla hivyo kulazimiska kuuahirisha hadi siku hiyo.
"Imetulazimu kuahirisha uchaguzi huo wa
netiboli Mkoa wa Dar es Salaam uliokuwa ufanyike kesho (leo) hadi Ijumaa
ijayo baada ya ukumbi tuliopanga kuutumia kutumika kwa shughuli
nyingine," alisema.
Aliwataka wajumbe wa mkutano huo wa uchaguzi
pamoja na wagombea kuwa wavumilivu na kujiandaa kwa mchakato huo katika
tarehe hiyo mpya iliyopangwa.
Halii aliwataja wagombea wanaowania nafasi
mbalimbali katika uchaguzi huo kuwa ni Winfrida Emmanuel (Mwenyekiti),
Pili Mogella (Makamu Mwenyekiti), Joseph Ng’aza (Katibu Mkuu), Christina
Mbetwa (Katibu Msaidizi), Anitha Lunogelo (Mhazini) na Michael Maurus
(Ofisa Habari).
Wajumbe ni Zainab Mohamed, Mathew Kambona, Mussa Sambala, Khadija Ally na Georgina Kasembe.
No comments :
Post a Comment