Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif Ali Iddi akisalimiana na
Wakala wa uuzaji wa Meli Kimataifa Bwana Rubin Rajan hapo nyumbani kwake
Mtaa wa Namanga Mjini Dar es salaam.
Kati kati ni Mfanyabiashara maarufu
Nchini ambaye pia ni Mbunge wa Singida Kaskazini Mh. Kassim Dewji.
Balozi wa Jamuhuri ya Cuba Nchini Tanzania Bwana Ernesto Gomez Pias
akimfariji Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif hapo nyumbani
kwake Mtaa wa Namanga Mjini Dar es salaam.
----
----
Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar iko tayari kutoa asilimia 20% ya mkopo
wa ununuzi wa Meli kubwa itakayokidhi mahitaji ya kusafirisha Abiria
na Mizigo kwa uhakika na salama kati ya Visiwa vya Zanzibar na Mwambao
wa Tanzania.
Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif Ali Iddi alieleza hayo
wakati akizungumza na Wakala wa mradi wa Paul Plan unaosimamia uuzaji
na ukopeshaji wa Meli kubwa za Abiria na Mizigo pamoja na Boti za uokozi
Bwana Rupin Rajan hapo Nyumbani kwake Mtaa wa Namanga Mjini Dar es
salaam.
Balozi Seif alisema Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar inachokiangalia
kwa hivi sasa ni kupata Usafiri wa uhakika utakaoondosha tatizo la
usafiri wa kubahatisha kwa wananchi kati ya maeneo hayo muhimu.
Alisema licha ya Serikali kukabiliwa na uhaba wa fedha za ununuzi wa
jumla lakini alimuomba wakala huyo kuhakikisha anatayarisha mapendekezo
yake ya namna atakavyokuwa tayari kukidhi mahitaji ya Zanzibar ya
kupata Meli kwa njia ya mkopo.
Balozi Seif alifahamisha kwamba Zanzibar ina Historia ndefu ya kuwa na
Meli zake kubwa za Serikali kabla na Baada ya Mapinduzi ambazo zilikuwa
zikihudumia Visiwa vya Zanzibar sambamba na mwambao wa Tanzania.
“ Huu mpango hata sasa hivi tungekuwa na uwezo wa kifedha
tungeurejesha kwa nia ya kuwahudumia Wananchi wetu bila ya matatizo”.
Alisisitiza Balozi Seif Ali Iddi.
Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar aliongeza kwamba fursa kwa Taasisi na
Makampuni ya Uwekezaji ipo lakini kinachozingatiwa zaidi na Serikali ni
kwa Muwekezaji kupelekea kabla mchanganuo wake Serikalini wa aina ya
Chombo anachotaka kuagiza kwa ajili ya uhakiki wa Kitaalamu.
Mapema Wakala huyo wa Mradi wa Paul Plan Bwana Rubin Rajan alimueleza
Balozi Seif kwamba Taasisi yake ina uwezo wa kuuza kwa jumla ya mkopo
vyombo ya usafiri wa abiria na mizigo katika nchi mbali mbali Duniani.
Alisema Taasisi hiyo imejipangia mipango ya kuuza vyombo vyao kwa njia
ya mkopo unaochukuwa takriban miaka 15 sambamba na boti za uokozi wakati
yanayotokea maafa.
Bwana Rubin alisema Taasisi hiyo kwa kutumia wataalamu wake pia
imekuwa na utaratibu wa kumtengenezea chombo cha Usafiri kama meli au
boti mteja wake kwa mujibu wa anavyohitaji kulingana na mazingira ya
bandari pamoja na kina cha maji ambacho chombo hicho kitatoa huduma
zake.
Wakati huo huo Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif Ali Iddi
alikutana na Balozi wa Cuba Nchini Tanzania Bwana Gonzale ambae alifika
nyumbani kwake Namanga kwa ajili ya kumpa pole kufuatia ajali ya Meliya
M.V Skagit iliyotokea wiki iliyopita na kusababisha vifo vya Watu
kadhaa.
Katika mazungumzo yao Balozi Seif ameipongeza Jamuhuri ya Cuba kwa hatua
zake za kuendelea kuiunga mkono Zanzibar kwenye harakati zake za
kiuchumi na ustawi wa Jamii.
Balozi Seif alisema
ushahidi wa hayo ameuona wakati wa ziara yake Nchini Cuba hivi karibuni
ambapo nchi hiyo imeonyesha nia ya kuendelea kuiunga mkono Zanzibar hasa
katika sekta ya Afya.
Alisema ukarimu wa Watu wa Cuba kupitia Balozi wa Nchi hiyo hapa
Tanzania umeongeza chachu ya ushirikiano sambamba na kuleta matumaini
hasa katika ile miradi inayoungwa mkono na Nchi hiyo rafiki.
“
Wataalamu na Madaktari wa Cuba waliopo Nchini wanaendelea kutoa huduma
vyema kwa Wananchi walio wengi Nchini”. Alifafanua Balozi Seif.
Naye Balozi wa Cuba Nchini Tanzania Bwana Ernesto GHomez Pias
alimuhakikishia Balozi Seif kwamba Cuba itaendelea kudumisha uhusiano wa
muda mrefu uliopo kati ya pande hizo mbili.
Bwana Gonzale
alisema hatua hiyo inathibitisha Madaktari 10 wa Tanzania wawili kati ya
hao kutoka Zanzibar wanaendelea kupatiwa mafunzo ya juu Nchini Cuba.
Na
Othman Khamis Ame,
Ofisi ya Makamu wa Pili wa Rais Zanzibar
No comments :
Post a Comment