![]()  | 
| Lulu 'Cindy | 
![]()  | 
| Marehemu Kanumba 'Mopao' enzi za uhai wake.. | 
Kutokana na mabadiliko hayo, Lulu ameepuka adhabu 
hiyo kwani hata kama atapatikana na hatia, adhabu yake ni kifungo cha 
maisha au kuachiwa huru.
Hii inatokana na kifungu cha 196 cha kanuni za 
adhabu ya kosa la kuua bila kukusudia, ambapo anayepatikana na hatia 
anaweza kuhukumiwa kifungo cha maisha, miaka kadhaa au kuachiwa huru.
Hata hivyo, baadhi ya wanasheria waliliambia 
gazeti hili kwamba uzoefu wa adhabu nyingi za kuua pasipo kukusudia 
zilizowahi kutolewa nchini, ni kati ya miaka 15 na wengine waliachiwa 
huru.
Lulu alifikishwa Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu, Aprili 11, mwaka huu akikabiliwa na tuhuma za kumuua Kanumba Aprili 7, 2012.
Alikuwa akidaiwa kutenda kosa hilo kinyume na 
kifungu cha 196 cha Sheria ya Mwenendo wa Makosa ya Jinai (CPA), shtaka 
ambalo mshtakiwa anayepatikana na hatia adhabu yake ni kunyongwa hadi 
kufa.
Hata hivyo, jana upande wa mashtaka ulieleza 
mahakamani kuwa kwa sasa imebadilisha mashtaka kutoka kuua kwa kukusudia
 na kuwa kuua bila kukusudia, kinyume cha kifungu cha 195 cha CP.
Mshtakiwa huyo alitarajiwa kusomewa mashtaka hayo 
mapya jana pamoja na maelezo yote ya kesi, ambapo angesomewa ushahidi wa
 mashahidi wote pamoja na vielelezo muhimu katika kesi hiyo.
Hata hivyo, hatua hiyo ilikwama kutokana na Wakili
 wa Serikali Mwandamizi, Tumaini Kweka anayeiendesha kesi hiyo 
kutokuwapo mahakamani na badala yake aliwakilishwa na Wakili wa 
Serikali, Ofmedy Mtenga.
“Upelelezi wa shauri lako umeshakamilika na 
tungeweza kukusomea comital (maelezo ya kesi) leo, lakini kwa kuwa 
waendesha mashtaka hawapo basi tunaliahirisha mpaka tarehe nyingine.”, 
alisema Hakimu Mkazi Agustina Mmbando, anayesikiliza kesi hiyo katika 
hatua hiyo ya awali.
Taarifa hizo za kukamilika kwa ushahidi wa kesi 
hiyo zilipokewa kwa furaha na shangwe na msanii huyo, kiasi kwamba 
alishindwa kujizuia kuonyesha furaha yake.
Wakili wake Peter Kibatala aliiomba mahakama itoe 
ahirisho fupi hadi Ijumaa kwa ajili ya mshtakiwa kusomewa mashtaka haya 
mapya pamoja na maelezo ya awali.Hakimu Mmbando alikubaliana na ombi hilo la Wakili Kibatala na akaahirisha kesi hiyo hadi Ijumaa.


No comments :
Post a Comment