Mkurugenzi wa wateja wakubwa wa kampuni ya simu za mkononi ya Zantel Ahmed Seif
Mohamed (kushoto ) akikabidhi mfano wa hundi yenye thamani ya Sh.6,040,000 kwa
Mwenyekiti wa chama cha Waandishi wa Habari za Michezo nchini (Taswa) Juma
Pinto, pembeni ya Mohamed ni Meneja Mwandamizi wa Mawasiliano na Masoko wa
Zantel Awaichi Mawala na Katibu Msaidizi wa Taswa, George John.
*****************************
KAMPUNI ya simu za
mkononi ya Zantel imejitokeza kudhamini Mkutano Mkuu wa Mwaka wa Chama cha
Waandishi wa Habari za Michezo Tanzania (TASWA) utakaofanyika Desemba 21 na 22
mwaka huu Kiromo View Resort Hotel, Bagamoyo mkoani
Pwani.
Akizungumza na
waandishi wa habari Dar es Salaam jana, Mkurugenzi wa Wateja Wakubwa wa Zantel
Ahmed Seif Mohamed, alisema wanajisikia furaha kushirikiana na TASWA kudhamini
mkutano huo wa aina yake.
Alisema Zantel
imekuwa na uhusiano mzuri na wanahabari, hivyo walipoombwa hawakusita kufanya
hivyo na wana matumaini makubwa utakuwa mkutano wenye manufaa.
Alieleza kuwa
kampuni yake baada ya kupata mafanikio katika mashindano ya Epiq Bongo Star
Search iliyomalizika hivi karibuni ni nafasi nyingine ya kuendelea kudhamini
matukio mbalimbali ya michezo na burudani kwa kadri uwezo
utakavyoruhusu.
Kwa upande
wake Mwenyekiti wa TASWA, Juma Pinto aliishukuru Zantel na kusema awali chama
hicho kiliomba udhamini kwa kampuni hiyo kwa lengo la kufanya mkutano Dar es
Salaam, lakini sasa walifikiria ufanyike Bagamoyo, Pwani.
Alisema Zantel
wamedhamini kwa kiasi cha Sh 6,040,000 na kwamba bajeti ya mkutano huo ni Sh
milioni 20, hivyo kuomba wadau wengine wasaidie ili kufanikisha mkutano huo
utakaohusisha zaidi ya waandishi wa habari za michezo 100 ambao ni wanachama wa
TASWA.
“Mkutano huo
unatarajiwa kushirikisha wanachama 100, na pia watakuwepo wadau mbalimbali wa
TASWA wakiwemo waandishi wakongwe wa habari za michezo wambao watapewa nafasi ya
kuzungumza kwenye mkutano huo,” alisema Pinto.
Kwa upande
wake Katibu Mkuu wa chama hicho,Amir Mhando aliwasisitiza wanachama kuendelea
kuthibitisha ushiriki wao na kuwa mwisho wa kufanya hivyo ni kesho
alasiri.
No comments :
Post a Comment