MWANASIASA
mkongwe nchini Alhaj Ramadhan Rashid Madabida pichani juu, ameishauri Jumuiya ya wanataaluma
wa Kiislamu nchini TAMPRO kuweka uwanja tambalale ili kuwawezesha vijana wasomi
wa Kiislamu kupata mwelekeo wa kimasomo na kimaisha kwa lengo la kujenga
ufanisi na maendeleo ya Taifa kwa ujumla wake.
Akizungumza
katika ufunguzi wa mkutano mkuu wa asasi hiyo isiyo ya kiserikali uliyofanyika
kwa siku mbili mfululizo jijini Dar es Salaam, Alhaj Madabida alisema Tampro
kwa kuwatumia wataalamu wao, inaweza kuanzisha kambi za vjana wenye vipaji maalum na kuwapa miongozo itakayowasaidia
kukabiliana na changamoto mbalimbali katika masomo yao.
“TAMPRO mnaweza
kuandaa kambi za vijana hasa wale walio kidato cha tano na sita na mkawashauri
mbinu na mikakati rafiki itakayowawezesha kufanya vizuri katika masomo yao,
kuliko kuwaacha kila mtu na lwake”, alisema Madabida.
Aidha Madabida
ambaye pia ni Mwenyekiti wa Chama cha Mapinduzi (CCM) Mkoa wa Dar es Salaam
aliwapongeza wanachama wa TAMPRO kwa upande wa kwanza na viongozi wake kwa
upande mwingine kwa kufanikiwa kukisimamisha chombo hicho ambacho alidai
matunda yake yameanza kuonekana.
“Ingawa
mnakabiliwa na changamoto nyingi na kwamba wapo wanaobeza jitihada zenu katika
kutelekeza malengo mliojiwekea, lakini ukweli unabaki palepale kwamba uwepo wa
TAMPRO ni faraja kwa jamii ya Waislamu
hapa nchini”, alisema.
Akaongeza kuwa,
uwepo wa taasisi hiyo ya wasomi ni faraja kwa jamii kwasababu inaonesha jinsi
vijana wa Kiislamu wanavyojitambua juu ya wajibu wao katika kupeleka mbele
maendeleo ya dini yao.
Naye Amir wa
TAMPRO Mussa Mzia ameitaka jamii ya waislamu kuipa ushirikiano jumuiya hiyo
katika harakati zake kwa kuwa moja ya malengo yake ni pamoja na kuihamasisha
jamii hiyo katika kujiendeleza kielimu na kujiletea maendeleo.
Aidha Mzia
akasema TAMPRO kama jumuiya ya wasomi wa Kiislamu, ina jukumu la kuwaunganisha
wataalamu wote wa dini hiyo na kujenga umoja na mshikamano baina yao na hivyo
akatoa wito kwa wasomi wa kujiunga na
asasi hiyo ili kutimiza malengo waliojiwekea ya kuanzisha miradi ya
maendeleo katika jamii ili jamii iweze
kujifunza kutokana na miradi hiyo.
|
No comments :
Post a Comment