Ndugu Wananchi,
Mtakumbuka kuwa hapo tarehe 23 Februari 2012 tuliwatangazia kupitia
vyombo vya habari juu ya usitishwaji wa matangazo ya televisheni kwa kutumia
teknolojia ya analojia kwenda katika mfumo mpya unaotumia teknolojia ya
dijitali.
Napenda kuwaleleza kuwa, maandalizi ya kuzima mitambo ya analojia
kuanzia tarehe 31 Desemba 2012 yamekamilika kwa mujibu wa makubaliano ya nchi
wanachama wa Jumuiya ya Afrika Mashariki.
Hata hivyo, napenda sasa kutoa taarifa kuwa uzimaji wa mitambo ya
analojia utafanyika kwa awamu kama ifuatavyo:-
(1) Dar Es Salaam-31 Desemba, 2012;
(2) Dodoma & Tanga- 31 Januari, 2013;
(3) Mwanza-28 Februari, 2013;
(4) Moshi & Arusha-31 Machi, 2013;
(5) Mbeya-30 Aprili, 2013.
Tumeamua kuanza kuzima mitambo hiyo kwa Jiji la Dar es Salaam kwanza ili
kutoa fursa kwa makampuni yenye leseni kusimika mitambo ya utangazaji wa
dijitali katika mikoa mingine. Makampuni haya yamejipanga kukamilisha usimikaji
wa mitambo hiyo katika mikoa minane katika miezi minane ijayo.
Mitambo ya analojia itakayozimwa kesho ni ile iliyopo Kisarawe na
Makongo. Vituo ambavyo siku ya tarehe 1 Januari 2013, vitapaswa kuanza
kutangaza matangazo kwa mfumo wa dijitali ni TBC1, ITV, EATV, Channel 10, StarTV,
DTV, CapitalTV, TumainiTV, ATN, MlimaniTV, C2C, CTN, CloudsTV na Efatha.
Mamlaka ya Mawasiliano Tanzania (TCRA) inafanya jitihada za kutosha
kuhakikisha kwamba makampuni yenye leseni za kusambaza ving’amuzi yanakuwa na
ving’amuzi vya kutosha na vingine vimeagizwa ili kukidhi mahitaji ya baadaye na
vile vilivyopo sokoni vina ubora unaokubalika.
Vilevile, Serikali kwa kushirikiana na Mamlaka ya Mawasiliano Tanzania
itahakikisha kwamba zoezi la uhamaji linafanyika bila usumbufu na kero kwa
wananchi. Makampuni yanayouza ving’amuzi yameagizwa yaimarishe huduma kwa
wateja wakati wa kuuza ving’amuzi na hata baada ya ununuzi iwapo wananchi
watakuwa na matatizo na ving’amuzi.
Zoezi hili la uhamaji ni muhimu sana kwa maendeleo ya nchi yetu.
Tutakapokuwa tumekamilisha uhamaji, huduma za mawasiliano na utangazaji
zitapanuka na kuwa bora zaidi. Kwa mfano, itawezekana sasa kuangalia
televisheni kupitia simu zetu za mikononi. Vilevile, itawezekana, kwa bei nafuu
kabisa, kwa mtu mwenye uwezo wa kutengeneza vipindi kukodisha chaneli yake na kutangaza
vipindi vyake. Vilevile, bei za mawasiliano na utangazaji zitashuka, na
tutakuwa tumepiga hatua kubwa kwenye mapinduzi ya teknolojia duniani, ambayo
nchi yetu haiwezi kubaki nyuma.
Ndugu Wananchi,
Serikali kwa kushirikiana na Mamlaka ya Mawasiliano Tanzania itaendelea
kutoa elimu kwa wananchi kuhusu uhamaji huu. Serikali inatarajia kupata
ushirikiano wa karibu kutoka kwa wadau wa sekta ya utangazaji na wananchi kwa
ujumla katika kipindi cha uzimaji wa mitambo ya utangazaji wa televisheni ili
kufanikisha zoezi la uzimaji wa mitambo ya utangazaji ya teknolojia ya
analojia.
Uhamaji huu hautahusu televisheni za wananchi zinazopata matangazo
kupitia madishi (nyungo) (satellite) au nyaya (cables). Hivyo, wananchi
wanaopata matangazo kupitia DStv, Zuku, na nyinginezo wataendelea kupata
matangazo yao kama kawaida.
Ndugu Wananchi
Kama kuna mwananchi yoyote ana kero, malalamiko, swali au anahitaji
maelekezo kuhusu uhamaji, awasiliane na Mamlaka ya Mawasiliano Tanzania (TCRA)
kupitia namba 0784-558270; 0784558271 au barua pepe: malalamiko@tcra.go.tz
Ndugu Wananchi,
Nawashukuru kwa kunisikiliza.
|
No comments :
Post a Comment