Na Anna Nkinda – Maelezo, Kagera
SERIKALI Mkoani Kagera imevikopesha vikundi  mbalimbali
 vya maendeleo vya vijana kupitia Vyama Vya Kuweka Akiba na Kukopa 
(SACCOS) zaidi ya shilingi milioni 83 katika kipindi cha miaka mitano 
iliyopita ili kuwawezesha vijana waweze  kujiajiri wenyewe na kujikwamua  kiuchumi .
Hayo yamesemwa leo na Mkuu wa Mkoa huo Kanali Mstaafu Fabian Massawe wakati akisoma taarifa fupi ya mkoa  kwa  Waziri wa Habari, Vijana, Utamaduni na Michezo Dk. Fenella Mukangara aliyepo mkoani humo kwa ajili ya kuangalia jinsi  fedha za mkopo kutoka mfuko wa vijana  zilivyoweza kuwasaidia vijana kujikwamua kimaisha.
Kanali Mstaafu Massawe alisema kuwa Serikali  inasimamia
 utekelezaji wa sera ya maendeleo ya vijana kwa kuratibu shughuli za 
mifuko ya vijana na kufuatilia utoaji na urejeshaji wa mikopo, 
kuhamasisha vijana na kufufua moyo wa kujitolea na kukuza na kuendeleza 
vipaji mbalimbali walivyonavyo vijana ili kuwawezesha kujiajiri kupitia 
mafunzo yanayohusu stadi za kazi na maisha
“Changamoto tunazokabiliana  nazo
 katika kuwakopesha vijana ni mahitaji makubwa ya mkopo ukilinganisha na
 uwezo wa SACCOS au wakopeshaji wengine, urejeshaji hafifu wa mikopo 
kutoka kwa wakopaji, ukosefu wa ajira, uvivu na uzurulaji, vijana kutaka
 mafanikio kwa haraka na matumizi ya madawa ya kulevya kwa baadhi ya vijana”, alisema Mkuu wa Mkoa huyo.
Aliendelea
 kusema kuwa ili kukabiliana na changamoto hizo Serikali ngazi ya mkoa 
inafuatilia kwa karibu ili kuona kwamba matamko ya sera ya Taifa ya 
Maendeleo ya vijana yanazingatiwa na kuingizwa katika  maendeleo
 ya Halmashauri lengo kuu ni mkoa kuwa na vijana wenye ari ya kuwajibika
 na kushiriki kikamilifu katika maendeleo ya jamii, wazalendo, wenye 
maadili na kupenda nchi yao.
Kwa
 upande wake waziri Dk. Mukangara alisema kuwa hivi sasa Serikali 
inaangalia uwezekano wa kuongea mkopo kwa SACCOS zinazolenga shughuli za
 maendeleo ya vijana  kutoka shilingi milioni tano hadi kumi kwani mahitaji ni makubwa na hayakidhi haja.
Dk. Mukangara alisema kuwa vijana  watumie
 fursa zinazowazunguka na kutambua kwamba ni wajibu wao na siyo jukumu 
la wazazi kuwakumbusha umuhimu wa kufanya kazi kwani ni aibu kijana kula
 chakula  bila ya kukitolea jasho huku mzazi akihangaika kufanya kazi.
“Vijana watambue kuwa fursa ya kupata ajira  ipo
 katika kero zinazowazunguka hivyo basi uongozi wa Serikali mkoani humu 
uwahamasishe vijana ili waweze kujiajiri na kuajiri kwani maendeleo ya 
Kagera yanawategemea wao hakuna mtu mwingine atakayeleta maendeleo yao”,
 alisema Waziri Dk. Mukangara.
Alimalizia
 kwa kuwataka viongoziwa Serikali kuwafuatilia vijana kwa ukaribu katika
 Kata na kuweza kuwafundisha na kuwashirikisha  katika
 miradi ya maendeleo ili waweze kusaidiana na jamii inayowazunguka kwa 
kushiriki ulinzi shirikishi, kupambana na tatizo la uhamiaji haramu na 
kufahamu umuhimu wa  utii wa sheria.
Mkoa
 wa Kagera unakadiriwa kuwa na idadi ya watu 2,739,492 kati ya hao 
wanawake 1,386,669 na wanaume 1,353,123 ambapo vijana ni 903,608 wenye 
umri wa miaka 15 hadi 35 sawa na asilimia 33 ya wakazi wote ambapo  kati ya hao wa kike ni 459,867 na wa kiume 443,741.

No comments :
Post a Comment