KONTENA lililosheheni kondomu za kiume kutoka nchini India
imekamatwa na kuzuiliwa katika Bandari ya Dar es Salaam, baada ya
kubainika kuwa hazifai kwa matumizi ya binadamu.
Maofisa wa Shirika la Viwango Tanzania (TBS)
wamelazimika kufanya msako mkali kwenye baadhi ya maduka ya dawa jijini
Dar es Salaam baada ya kubainika kwamba tayari kondomu hizo zipo sokoni.
Akizungumza na waandishi wa habari jana Dar es
Salaam, Kaimu Mkurugenzi Mkuu wa TBS, Leandri Kinabo alizitaja kondomu
hizo kuwa ni aina ya Melt Me zenye thamani ya Sh222.1 milioni
zilizokamatwa tangu Oktoba 23 mwaka huu na kuzuiliwa bandarini hapo kwa
taratibu zaidi za kisheria.
“Jambo lililotushtua ni kwamba zimebainika kwamba
zipo madukani, tukajaribu kufuatilia tena bandarini tukifikiri kuwa
huenda zimetolewa kinyemela licha ya kuzuiliwa ili ziteketezwe au
zirejeshwe nchini India kwa gharama zao wahusika.
Tulipokwenda bandarini tukabaini kwamba bado zipo
katika hali ile ile, kumbe zimeingizwa nchini kwa njia ya panya, kwa
kweli ni mbovu na ndiyo maana tumelazimika kuwajulisha wanahabari ili
muwape taarifa wananchi wawe makini,” alisema Kinabo.
Alifafanua zaidi kwamba kondomu hizo ni mbovu
kwani zimebainika kuwa na vitundu, pia zinapasuka haraka, hazina kabisa
viwango vya ubora wa bidhaa unaotakiwa na Shirika la Viwango la
Kimataifa (ISO).
Kinabo alisema kuwa TBS bado wanaendelea kufanya
mawasiliano na kampuni iliyotengeneza kondomu hizo, lakini kwenye kasha
lake inaonyesha kuwa inaingizwa nchini na kampuni ya Fair Deal Exim ya
Dar es Salaam.
|
No comments :
Post a Comment